Friday, July 1, 2016
MJADALA WA SAKATA LA LUGUMI WAZIKWA RASMI.......NAIBU SPIKA AIPA SERIKALI MIEZI MITATU.
Do you like this story?
Kiu ya
wabunge kujadili sakata la utekelezwa mbovu wa mkataba baina ya Jeshi la Polisi
na kampuni ya Lugumi Enteprises Limited, imezimwa baada Naibu Spika, Dk Tulia
Ackson kuiagiza Serikali kukamilisha utekelezaji wa mradi huo ndani ya miezi
mitatu ijayo.
Kwa muda
mrefu, wabunge walikuwa wakisubiri ripoti ya uchunguzi kutoka Kamati ya Hesabu
za Mashirika ya Umma (PAC) ili waweze kujadili kwa kina sakata hilo
linalohusisha mradi wa Sh37 bilioni wa kufunga vifaa vya kielektroniki vya
kuchukua alama za vidole (AFIS).
Mapema
Aprili mwaka huu, wakati PAC ikipitia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka ulioshia Juni 30, 2014 ilibaini kuwa Lugumi
ilikuwa imefunga mashine katika vituo 14 tu kati ya 108 ilivyotakiwa kuvifunga
wakati ikiwa imeshapokea asilimia 99 ya malipo yote.
PAC
ilimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani apeleke taarifa ya
utekelezaji wa mradi huo ambayo aliipeleka Aprili 18 na kubaini kuwa vifaa
hivyo vilifungwa katika vituo 153 pamoja na makao makuu ya polisi.
Kutokana
na utofauti wa takwimu za CAG na PAC iliunda kamati ndogo kufanya uhakiki wa
vifaa vya AFIS na sababu za kuchelewa kutekelezwa kwa mradi, huku wengi
wakitarajia ripoti hiyo ingejadiliwa bungeni.
Katika
sakata hilo, wabunge walimtuhumu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles
Kitwanga kuwa na masilahi kwa madai kuwa alikuwa mmoja wa wanahisa wa kampuni
ya Infosys iliyoshirikishwa kwenye mradi huo na kushinikiza ajiuzulu kupisha
uchunguzi.
Hata
hivyo, Kitwanga alitimuliwa kazi kwa kosa jingine la kuingia bungeni kujibu
maswali ya wizara yake akiwa amelewa.
Jana, Dk
Tulia alitumia kanuni 117(17) kukabidhi matokeo ya uhakiki huo kwa Serikali,
yakiwemo maoni, ushauri, mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto
zilizoanishwa na taarifa ya kamati ya PAC na kutoruhusu mjadala kwa wabunge
Dk Tulia
alieleza kuwa amefanya uamuzi huo baada ya kupokea taarifa hiyo na kuangalia
maudhui yake, kuzingatia matokeo ya uhakiki huo uliofanywa na kamati ndogo na
PAC kujiridhisha uwepo wa vifaa hivyo, ukiacha kasoro zilizojitokeza.
Pia, alisema suala hilo si jipya kwa
kuwa linatokana na hoja ya ukaguzi wa miaka ya nyuma na kilichokuwa kimebaki ni
vifaa hivyo kufanya kazi.
“Naagiza
sasa kwamba Serikali ihakikishe mfumo huu unafanya kazi ndani ya miezi mitatu
kuanzia leo (jana) ili kuboresha uwezo wa Jeshi la Polisi kuwa na utambuzi wa
haraka wa wahusika wa matukio ya kihalifu katika vituo vyote nchini,” alisema huku akishangiliwa.
Dk Tulia aliitaka pia Serikali kuyapatia ufumbuzi haraka masuala yote yaliyobainika kuwa na dosari za kiutendaji.
Dk Tulia aliitaka pia Serikali kuyapatia ufumbuzi haraka masuala yote yaliyobainika kuwa na dosari za kiutendaji.
Alisema
ameielekeza kamati ya PAC kuhakiki maagizo aliyoyatoa kwa Serikali na baada ya
uhakiki huo itoe taarifa bungeni wakati ikiwasilisha taarifa yake ya mwaka.
“Natarajia
kuwa suala hili sasa litafikia mwisho na CAG atafunga hoja yake baada ya
kujiridhisha na utekelezaji wa maagizo niliyoyatoa,” alisema Dk Tulia.
Mwenyekiti
wa PAC, Aeshi Hilaly alisema walishamaliza kazi yao baada kumkabidhi Naibu
Spika ripoti hiyo, kama kanuni zinavyotaka na kwamba yeye ndiye mwenye uamuzi
wa mwisho.
Aliyekuwa
mwenyekiti wa kamati hiyo ndogo ya kuchunguza suala hilo, Japhet Asunga alisema
baada ya uchunguzi, walibaini vituo 15 tu kati ya 153 ndivyo vimeunganishwa na
mfumo wa taarifa za polisi.
Asunga,
ambaye ni mbunge wa Vwawa (CCM), alimwambia mwandishi wetu kuwa kamati ilibaini
kuwa vifaa vyote vya AFIS vilivyokuwapo katika vituo vimetelekezwa bila
kuunganishwa katika mfumo wa mtandao.
Alisema
sehemu nyingine walikuta vifaa vimetupwa huku vingine vimeharibika kwa sababu
vimekaa muda mrefu kama wino wa printa umeisha muda wake.
“Tumeagiza
Serikali ichukue hatua stahiki kuhakikisha vifaa vinatumika na kuwaadhibu wote
waliochelewesha na nani hakufanya kazi ipasavyo.
“Ndiyo
maana Naibu Spika baada kupima maagizo yaliyotolewa ameona Serikali ianze
kuyafanyia kazi mapungufu badala ya kusubiri kuyawasilisha Septemba. Naona
busara imetumika,” alisema Asunga.
Alisema
kamati haina tatizo na maazimio ya miezi mitatu aliyotoa Spika kwa kuwa ndiyo
mapendekezo yao na kwamba PAC wao awali walipendekeza miezi sita.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MJADALA WA SAKATA LA LUGUMI WAZIKWA RASMI.......NAIBU SPIKA AIPA SERIKALI MIEZI MITATU.”
Post a Comment