Friday, September 16, 2016

KUELEKEA KWENYE DEBY YA MBEYA CITY Vs TANZANIA PRISONS KESHO, HIKI NDIO WALICHOKISEMA MBEYA CITY.




ZIKIWA zimebaki saa chache kabla ya kuchezwa  kwa mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara  unaozikutanisha  Mbeya City Fc na Tanzania  Prison,maandalizi kuelekea  mchezo huo  uliopangwa kuchezwa kwenye uwanja wa  Sokoine jijini hapa  yamekamilika.

Akizungumza mbele ya wana habari  muda  mchache  uliopita,  afisa  habari wa City, Dismas Ten, amesema  kuwa maandalizi ya kikosi chake  kuelekea mchezo huo  uliopangwa kuchezwa  jumamosi hii saambamba na  michezo mingine mitano itakayorindima kwenye viwanja tofauti tayari yamekamilika na kinachosubiliwa na dakika 90 hiyo kesho.

“Kesho ni siku ya mchezo, kwetu sisi huu ni mchezo muhimu kwa sababu tunahitaji kushinda ili tuendelee kuwepo kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi, maandalizi ya kutosha yamefanyika kwa hiyo ni nafasi kwa mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kusapoti timu yao,jopo la madaktari wetu limenithibitishia kuwa  Geoffrey Mlawa  hatakuwepo uwanjani hiyo kesho lakini nyota wengine wako kwenye hali nzuri, huu ni msimu ambao  City inarudi kwenye zama  zake” alisema.

Kuhusu utulivu na amani uwanjani kwa mashabiki watakaojitokeza  kushuhudia mchezo huo, Ten alisema kuwa  watu wanatakiwa kuzingatia amani kwa sababu mchezo wa soka hukutanisha watu wengi hivyo ni vyema  mashabiki kushangilia timu zao  huku wakiwa kwenye hali nzuri ya amani.

“Mashabiki  wa  City  wajitokeze kwa wingi, wasiwe na shaka ya utulivu kwa sababu ulinzi  utakuwepo wa kutosha, amani mchezoni ni jambo jema  hivyo kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake  kuhakikisha  tunashangilia timu yetu vizuri katika kuhanikiza ushindi huku tukiwa na wingi wa amani”  alimaliza.

City inakutana na Prison huu ukiwa ni mchezo wa 7 kwenye mfululizo wa mechi za ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara huku rekodi zikionyesha kuwa City imepata ushindi mara 2, Prison wakishinda mara 3 na mara 1 timu hizi zikienda  sare, Kiungo Peter Mapunda ndiye mchezaji anashika rekodi ya kufunga bao la kwanza kabisa kwenye mechi zilizokutanisha timu hizi mbili akifunga bao hilo kwenye mchezo wa duru ya kwanza msimu wa 2013/14  kwenye ushindi wa 2-0, misimu itatu iliyopita.

0 Responses to “KUELEKEA KWENYE DEBY YA MBEYA CITY Vs TANZANIA PRISONS KESHO, HIKI NDIO WALICHOKISEMA MBEYA CITY.”

Post a Comment

More to Read