Friday, September 16, 2016
WAZIRI MKUU AFUNGA BUNGE AWAOMBA WATANZANIA KUWACHANGIA WAHANGA WA TETEMEKO LA ARDHI, KAGERA
Do you like this story?
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amehitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge la
Kumi na Mbili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Mjini Dodoma.
Akihitimisha
Bunge, Waziri Mkuu ameainisha mambo mbalimbali ambayo yamefanyika wakati wa
Mkutano huo ikiwa ni pamoja na mijadala mbalimbali inayohusu miswada ya sheria
iliyosomwa kwa mara ya kwanza, mara pili na kwa mara ya tatu.
Waziri
Mkuu amesema kuwa mijadala ya mkutano huo ilikuwa ya uwazi na hoja zilizotolewa
zililenga katika kuleta maendeleo nchini.
“Nawapongeza
sana wabunge wote kutokana na michango yenu mizuri na yenye tija hatua ambayo
ilibidi mara kadhaa vikao vyetu kuendelea hadi usiku ikiwa ni nje ya muda wa
kanuni za Bunge,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Katika kuhitimisha mkutano huo, Waziri Mkuu amebainisha baadhi ya matukio mbalimbali yaliyotokea nchini ikiwemo janga la tetemeko la ardhi, shughuli za bunge, mwenendo na mwelekeo wa hali ya uchumi, mwenendo wa ukusanyaji mapato ya Serikali, mpango wa Serikali kuhamia Dodoma, hali ya upatikanaji wa chakula nchini, maboresho katika tasnia ya Ushirika, Sekta ya elimu, suala la uhakiki wa vyeti kwa watumishi, kuimarisha usafiri wa anga, hali ya amani na utulivu nchini pamoja na suala la michezo nchini.
Akizungumzia
kuhusu janga la tetemeko la ardhi lililotokea mikoa ya Kanda ya Ziwa, Waziri
Mkuu ametoa wito kwa wananchi, Sekta binafsi na Jumuiya za Kimataifa kuendelea
kushirikiana na Serikali katika kusaidia waathirika wa tetemeko hilo.
“Serikali
inaendelea kukusanya michango kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali,
waliotayari kuchangia wanaweza kutumia akaunti ya maafa iliyofunguliwa benki ya
CRDB yenye namba 0152225617300 kwa jina la Kamati ya Maafa Kagera na kwa njia
ya simu michango hiyo inaweza kutumwa pia kupitia M-pesa 0768-196669, Airtel
Money 0682-950009 na Tigo pesa 0718-069616” amesisitiza Waziri Mkuu.
Kwa
upande wa mwenendo na mwelekeo wa hali ya uchumi nchini, Waziri Mkuu amesema
kuwa kwa ujumla hali ya uchumi nchini inaridhisha na inaendelea kuimarika.
Kwa
mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) hali ya uchumi umeimarika ambapo pato la
Taifa lilikua asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kwa mwaka 2015,
ukuaji huo unatoka na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, huduma za
mawasiliano, utangazaji na huduma za intaneti na kuongezeka kwa uchimbaji wa
madini.
Katika
suala la ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa mwezi Julai na Agosti, Waziri
Mkuu amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi hicho mapato
yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalikuwa shilingi Trilioni
2.168 ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi trilioni 2.113 ikiwa ni
sawa na ongezeko la asilimia 103 ya lengo la Serikali.
Waziri
Mkuu amesema kuwa, katika mpango wa Serikali kuhamia Dodoma ni dhamira ya
Serikali ya Awamu ya tano ya kukamilisha mchakato na ahadi ya Serikali ya
kuhamia katika Mji wa Makao Makuu Dodoma ambapo utekelezaji wake utakuwa wa
awamu sita.
Vilevile
katika sekta ya Kilimo, Waziri Mkuu amesema kuwa hali uzalishaji na upatikanaji
wa chakula nchini umefika tani 16,172,841, ambapo Serikali imetoa ruzuku za
pembejeo za kilimo kwa ajili ya mazao ya chakula hususani mahindi, mpunga na
mtama, kwa upande wa mazao ya biashara ruzuku hiyo hutolewa katoka mazao ya
korosho, pamba, chai, kahawa na alizeti.
Pia
Serikali itafanya marekebisho ndani ya tume ya maendeleo ya Ushirika na
kuchukua hatua za kinidhamu kwa watakao bainika na ubadhirifu wa mali za
ushirika.
Katika
Sekta ya Elimu, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali imeamua walimu wapya
watakaoajiriwa wapangiwe vituo vya kazi moja kwa moja na kwa kuzingatia maeneo
yenye upungufu wa walimu.
Kuhusu
uhakiki wa vyeti vya watumishi, Waziri Mkuu amesema kuwa, Serikali inaendelea
na zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi na kuwaagiza wagurugenzi wa
halmashauri kuandaa vituo maalum ambavyo vipo jirani na vituo vya kazi ili
kuwapunguzia watumishi gharama na adha wakati wa zoezi hilo.
Katika
kuboresha usafiri wa anga nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imenunua
ndege mbili aina ya Dash 8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja
zitakazotumika kutoa huduma za usafiri wa anga kwa soko la ndani na chi jirani.
Hata
hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa vyombo vya usalama na ulinzi nchini vimeendelea
kulinda na kudumisha amani na utulivu nchini kwa manufaa ya ustawi wa nchi ili
kufanikisha lengo la kukuza uchumi na kuondoa umaskini.
Aidha,
Waziri Mkuu ameipongeza Timu ya Taifa ya Vijana Serengeti Boys kwa kuiwakilisha
vyema Tanzania katika mashindano ya Kimataifa.
Mbali na
hayo Waziri Mkuu Majaliwa amepokea michango mbalimbali iliyotolewa na Kampuni
ya Caspian shilingi milioni 100, Ofisi ya Taifa ya Takwimu shilinhi milioni 1.6
na kampuni ya Bordar Ltd shilingi milioni 20 kwa ajili ya waadhirika wa
tetemeko lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Na
Beatrice Lyimo na Eleuteri Mangi – MAELEZO, Dodoma
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WAZIRI MKUU AFUNGA BUNGE AWAOMBA WATANZANIA KUWACHANGIA WAHANGA WA TETEMEKO LA ARDHI, KAGERA ”
Post a Comment