Wednesday, September 14, 2016
MWENYEKITI WA BUNGE AMUOMBA RADHI MBOWE BUNGENI
Do you like this story?
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu
amemuomba radhi kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kwa
kushindwa kutambua mchango wake kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani
Kagera.
Hatua hiyo imefutia mwongozo ulioombwa
na wabunge wawili Chadema, kuwa mchango wa Mbowe haukutambulika licha ya kufika
Bukoba, kutoa misaada na kushirikiana na waathirika wa tukio hilo hadi sasa.
Aliyeanza kuomba mwongozo ni Mbunge wa
Tarime Vijijini, John Heche ambaye alihoji kwa nini mwenyekiti huyo wa Bunge
amewatambua viongozi waliofika eneo la tukio na kutoa misaada lakini ameshindwa
kumtambua Mbowe ambaye mpaka sasa yupo eneo la tukio na ametoa msaada.
Mbunge mwingine ni Pascal Haonga wa
Mbozi ambaye alisema Mbowe ni kiongozi mkubwa na halitakuwa jambo la maana kama
mchango wake hautatambulika kwani suala hilo siyo la kisiasa.
Kufuatia mwongozo huo, Zungu aliomba
radhi na kuongeza kuwa anamtambua Mbowe kama kiongozi aliyetoa msaada kwa
waathirika hao.
Awali, Mwenyekiti huyo wa Bunge baada
ya kuingia ukumbini alitoa pole kwa waathirika wa tetemeko hilo lililoua watu
17 na kuwatambua watu waliochangia tukio hilo akiwamo Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa na wafanyabiashara.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu
kuisha, mwenyekiti huyo aliwatambua wafanyabiashara wengine waliotoa msaada kwa
waathirika hao lakini hakugusia msaada ulitolewa na Mbowe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MWENYEKITI WA BUNGE AMUOMBA RADHI MBOWE BUNGENI”
Post a Comment