Wednesday, October 19, 2016

JANUARY MAKAMBA:KUANZIA MWAKANI WANAFUNZI WOTE DARASA LA KWANZA KUKABIDHIWA MTI MMOJA KWA AJILI YA KUUTUNZA.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe January Makamba pamoja na wanafunzi wakipanda Mti.




Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe January Makamba akimwagia Mti alioupanda.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe January Makamba akimpa maelezo Mwanafunzi jinsi ya kutunza Mazingira.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe January Makamba amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuanzia mwakani itatoa maagizo kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anayeanza darasa la kwanza katika shule za serikali na zile za binafsi atahitajika kufika shuleni na mche mmoja wa mti siku  ya kuanza masomo ikiwa kama moja ya mahitaji ya msingi na kwa upande wa wanafunzi wa sekondari watapaswa kufika na miche mitatu wakati wa kuanza masomo.

Waziri Makamba ameainisha kwamba maelekezo yatapelekwa Wizara ya Elimu na TAMISEMI na moja ya mahitaji ya kupewa cheti cha kuhitimu ni kukabidhi miti iliyopandwa wakati mwanafunzi anaingia kuanza masomo hivyo atahitajika kutunza na kuhudumia miti hiyo kipindi chote cha masomo.

Waziri Makamba ameyasema hayo wakati akishiriki zoezi la upandaji miti na wanafunzi katika Shule ya Msingi Mlandege iliyopo katika Kata ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa ambapo aliongozana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Iringa. Waziri Makamba ametanabaisha kuwa lengo la kushiriki zoezi la upandaji miti pamoja na wanafunzi  hao ni kutuma ujumbe mahsusi na wa uhakika kabisa kwamba uhifadhi,usimamizi na utunzaji wa Mazingira ni jukumu la msingi kwa manufaa ya kizazi kinachokuja na ndio sababu hasa ya kushiriki na wanafunzi ili waweze kujifunza na kuelewa.

Waziri Makamba ameainisha kuwa katika shule zenye uhaba wa maeneo yanayoweza kutumika kwa upandaji miti, maeneo mbadala yatakayoelekezwa na serikali za vijiji na mitaa.

Waziri huyo mwenye dhamana ya Mazingira amesema hili linafanyika ikiwa ni moja kati ya hatua mahsusi,  stahiki na za maksudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuendana na mabadiliko ya tabia nchi hasa ikizingatiwa kuwa asilimia 61 ya nchi yetu ipo katika tishio la kuwa  jangwa.

Vilevile Waziri Makamba amesema kuwa kuanzia tarehe 5-6 Novemba Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti na Mameya wote watakutana Jijini Arusha Kwaajili ya kupata mafunzo na maelekezo mahsusi yanayohusiana na Hifadhi ya Mazingira, ikiwemo upandaji miti na utunzaji wa vyanzo vya maji

0 Responses to “ JANUARY MAKAMBA:KUANZIA MWAKANI WANAFUNZI WOTE DARASA LA KWANZA KUKABIDHIWA MTI MMOJA KWA AJILI YA KUUTUNZA.”

Post a Comment

More to Read