Tuesday, October 4, 2016
MALINZI: SITAWAACHA SERENGETI BOYS LICHA YA KUONDOLEWA NA CONGO
Do you like this story?
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema kwamba ataendelea kuwa karibu na vijana
na Timu ya Tanzania ya vijana ‘Serengeti Boys’ licha ya kuondolewa na Congo
kwenye harakati za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana
zitakazofanyika Madagascar, hapo Aprili, mwakani.
Mipango ya TFF kwa sasa inayoongozwa na
Malinzi kwa sasa ni kuiiingiza timu hiyo kwenye program ya timu ya vijana wenye
umri wa chini ya miaka 20 maarufu kwa jina la Ngorongoro Heroes baada ya
kuguswa na kilio cha vijana hao ambao walishindwa kujizuia kumwaga machozi
mbele ya Malinzi ambaye alifanya kazi kubwa kuwatuliza pamoja na viongozi
wengine.
Serengeti Boys ilipoteza mchezo dhidi ya
Congo Oktoba 2, 2016. Kwa kupoteza mchezo huo dakika ya pili kati ya nne ya
nyongeza baada ya kumalizika kwa dakika 90, kumefanya vijana hao wa Tanzania
kuenguliwa kwenye mashindano ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika – fainali zitakazofanyika Madagascar.
Dakika moja ndiyo iliyoipoteza Serengeti
Boys kufuzu kwa fainali hizo kwa bao la dakika ya 92 la lililofungwa na Mountou
Edoward.
“Niko nanyi, najua mna group la
WhatsApp, naomba msifute namba yangu. Iwe humo na mambo yenu mengi naomba
mniambie humo, na nitayashughulikia iwe binafsi au kiofisi. Nawahakikishia
sitawaacha,” alisema Malinzi alipowafariji vijana hao ambao wanatarajiwa
kuingia leo saa 3.00 usiku huu kwa ndege ya Shirika la Ndege ya Rwanda.
“Umri wenu bado sana wa kucheza soka.
Program za TFF, CAF na FIFA ziko nyingi pia mnaweza kupata nafasi ya kucheza
Olimpiki na kuna michuano mingi, sitawaacha,” alisema Malinzi na kusisitiza ana
imani na timu hiyo ambayo kwa dakika 90 za mchezo dhidi ya Congo walipambana kwelikweli
kutetea taifa lao pendwa Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MALINZI: SITAWAACHA SERENGETI BOYS LICHA YA KUONDOLEWA NA CONGO”
Post a Comment