Tuesday, October 4, 2016

ETHIOPIA YAFUTA MCHEZO WA KIRAFIKI NA TANZANIA




Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea barua kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Ethiopia (EFF), ikielezea juu ya kufutwa kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliokuwa ufanyike Oktoba 8, 2016.

EFF imesema kwamba imelazimika kufuta mchezo huo ulikuwa kwenye kalenda ya FIFA kwa sababu za hali ya hewa si rafiki kwa sasa nchini Ethiopia.

Kwa barua hiyo, Kocha Mkuu wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania (Taifa Stars), Charles Boniface Mkwasa atalazimika kuvunja kambi ya timu hiyo ambayo iliweka kwenye Hoteli ya Blue Pear iliyoko Ubungo, Dar es Salaam.

Mchezo huo uliratibiwa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo huwa na kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa kwa wanachama wake – Tanzania ni miongoni mwao. EFF, ndio walioomba nafasi hiyo.
Ingekuwa ni faida kwa Tanzania kama ingeshinda mchezo huo kwa maana kina alama za nyongeza kama inatokea unaifunga timu mwenyeji.

Matokeo yake yangekuwa ni sehemu malumu kupima viwango vya ubora na uwezo wa timu za taifa. Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 132 kati ya nchi 205 wanachama wa FIFA zilizopimwa ubora. Ethiopia yenyewe inashika nafasi ya 126.

Argentina inaongoza ikifuatiwa na Ubelgiji anakocheza Mbwana Samatta – nyota wa kimataifa wa Tanzania. Samatta anacheza klabu ya K.R.C Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji.

 Timu nyingine bora kimataifa ni Ujerumani, Colombia na Brazil.

Katika Bara la Afrika, Ivory Coast ambayo ni ya 34 kwa ubora duniani ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na Algeria, Senegal, Tunisia na Ghana.

0 Responses to “ ETHIOPIA YAFUTA MCHEZO WA KIRAFIKI NA TANZANIA”

Post a Comment

More to Read