Tuesday, October 4, 2016
RAIS KABILA WA CONGO-DRC AWEKA JIWE LA MSINGI BANDARINI JIJINI DAR ES SALAAM
Do you like this story?
Rais
wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Joseph Kabila Kabange ameweka jiwe la
msingi la jengo la Kituo cha Pamoja cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania (TPA) ambalo limejengwa kwa lengo la kuwaweka pamoja wadau wote
wanaotoa huduma katika bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni juhudi za kuboresha
huduma na kupunguza gharama kwa watumiaji wa bandari hiyo.
Hafla ya uwekaji jiwe la msingi la jengo hilo refu kuliko yote Afrika Mashariki na kati imefanyika leo tarehe 04 Oktoba, 2016 na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
Akizungumza
kabla ya kuwekwa jiwe hilo la msingi Rais Magufuli ameishukuru Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwa mteja mkubwa wa bandari ya Dar es Salaam na
amesema aliamua jiwe la msingi la jengo hilo liwekwe na Rais wa Kongo kwa
kutambua umuhimu wa nchi yake katika biashara ya bandari ya Dar es Salaam na
pia undugu na urafiki wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizi mbili.
Rais
Magufuli amemhakikishia Rais Kabila kuwa kama ambavyo Serikali yake imechukua
hatua kadhaa za kurekebisha kasoro zilizokuwepo katika bandari hiyo, itaendelea
kujenga mazingira mazuri zaidi kwa wafanyabiashara wa Kongo kutumia bandari
hiyo ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa, kuongeza muda wa kutunza
mizigo inayoshushwa kutoka siku 14 hadi siku 30, kuanzisha bandari kavu katika
eneo la Ruvu mkoani Pwani na kuinua ari ya wafanyakazi wa bandari kutoa huduma
bora.
"Mhe.
Rais Kabila bandari yetu ilifikia mahali pa kuandika rekodi ya kupotea kwa meli
kwenye taarifa za bandari, kuna wakati hapa zilipotea meli 60, lakini pia
mizigo ya watu ilikuwa inapotea na wafanyabiashara walikuwa wanaombwa rushwa.
"Kuna
baadhi ya wafanyakazi wa bandari waliifanya hii bandari kama mali yao, walikuwa
wanaondoka na fedha za rushwa kwenye buti za magari, naomba nikuhakikishie kuwa
haya hayatatokea tena, na yakitokea Mhe. Balozi wa Kongo upo hapa njoo unieleze
mimi au mwambie Makamu wa Rais au Waziri Mkuu" amesisitiza Rais Magufuli.
Dkt.
Magufuli pia amempongeza Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete kwa kuanzisha ujenzi wa jengo hilo la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania na kwamba anaamini litasaidia kuimarisha biashara kati ya Tanzania na
Kongo na nchi nyingine zinazotumia bandari ya Dar es Salaam.
Kwa
upande wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Joseph Kabila Kabange
amemshukuru Rais Magufuli kwa heshimu kubwa aliyompa yeye na nchi ya Kongo ya
kuweka jiwe la msingi la jengo hilo na amesema kutokana na Tanzania kuchukua
hatua madhubuti za kuimarisha huduma za bandari ya Dar es Salaam mizigo ya
Kongo itapitia bandari hiyo.
"Mhe.
Rais Magufuli bandari hii ipo Dar es Salaam lakini bandari hii ni ya kwetu
sote, mashariki ya Kongo inapakana na nchi nne za Tanzania, Rwanda, Burundi na
Uganda lakini asilimia 50 ya mizigo inatoka Tanzania hususani katika bandari ya
Dar es Salaam.
"Nimefurahi
pia kuwa katika juhudi za Tanzania kuboresha bandari pia mnaboresha barabara na
bandari ndogo ndogo za ziwa Tanganyika, hili ni jambo muhimu kwa sababu sasa
mizigo ya Kongo itasafiri kwa urahisi na wafanyabishara wa Kongo waliokuwa
wameacha kutumia bandari ya Dar es Salaam watarudi" amesema Rais Kabila.
Mhe.
Joseph Kabila Kabange amesema katika miaka ya 70 na 80 Kongo ilikuwa ikizalisha
shaba kiasi cha tani laki 1 lakini hivi sasa inazalisha hadi tani Milioni 1.2
na zote hizi zinategemewa kusafirishwa nje ya nchi kupitia bandari ya Dar es
Salaam.
Ameipongeza
Serikali ya Tanzania kwa kununua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 na ameunga
mkono mpango wa kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na Kongo
huku akibainisha kuwa nchi yake pia itanunua ndege kwa ajili ya kuimarisha
zaidi usafiri wa anga kati ya nchi hizi mbili.
Mapema
kabla ya Marais wote wawili kuzungumza, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi
wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deodatus Kakoko alisema jengo hilo lina
ghorofa 35, urefu wa meta 157, ukubwa wa meta za mraba 65,115 na ujenzi wake
unatarajiwa kukamilika tarehe 31 Desemba, 2016 kwa gharama ya Shilingi Bilioni
130.
Rais
Kabila ambaye aliingia hapa nchini jana tarehe 03 Oktoba, 2016 kwa ziara ya
kiserikali ya siku tatu, jioni ya leo atahudhuria dhifa ya kitaifa katika
ukumbi wa Ikulu Jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa kwa ajili yake na Mwenyeji
wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar
es Salaam
04
Oktoba, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ RAIS KABILA WA CONGO-DRC AWEKA JIWE LA MSINGI BANDARINI JIJINI DAR ES SALAAM”
Post a Comment