Tuesday, October 18, 2016
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Afikishwa Mahakamani Kwa Kosa La Kumtishia Bastola Askari wa Usalama Barabarani (Trafiki)
Do you like this story?
Ilikuwa
kama mchezo wa kuigiza kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro baada ya Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Emmanuel Mkumbo kufikishwa ili
apandishwe kizimbani kujibu mashtaka sita, likiwamo la kutishia kuua.
Tukio
zima la kumpeleka mahakamani, kumpandisha kizimbani na kumsomea mashtaka kwa
muda wa dakika 30 hivi lilitawaliwa na vituko. Kwanza, ni jaribio la kuwaficha
wanahabari.
Kabla
ya kufikishwa mahakamani, Polisi mkoani Morogoro iliwaarifu wanahabari kuwa
ingetoa taarifa kuhusu mkurugenzi huyo lakini saa 4:30 asubuhi wakati Kamanda
wa Polisi mkoani Morogoro, Ulrich Matei akijiandaa kuzungumza nao, alipigiwa
simu akatoka nje ya ukumbi na aliporejea alisema hawezi kutoa taarifa tena na
akaondoka.
Waandishi
walipofika mahakamani saa 5:00 asubuhi walikuta Kamanda Matei akishuka kwenye
gari na alipanda tena akasogea kando kuzungumza na baadhi ya askari wake.
Pili,
baada ya hakimu kumaliza kusikiliza kesi hiyo, Mkumbo hakurudishwa mahabusu
mahakamani hapo kama ilivyo ada ili kusubiri utaratibu mwingine badala yake
mshtakiwa huyo alihamishiwa chumba cha hakimu ambacho hakikuwa na kesi
inayoendelea.
Humo
ndugu zake walimpelekea koti kubwa jeusi na kofia aina ya pama, hivyo alitoka
akiwa tofauti na alivyoingia akiwa na fulana yenye rangi nyeupe, bluu na
nyeusi. Baada ya kuvaa alitoka akiwa amezingirwa na polisi, huku ndugu
wakiwazuia wanahabari kumpiga picha.
Mashtaka
dhidi yake
Mkumbo
ambaye ni mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam alipandishwa kizimbani kujibu
mashtaka sita, la kwanza likiwa la kutishia kuua kwa bastola na la pili ni la
usalama barabarani lenye makosa matano.
Alisomewa
mashtaka hayo na mawakili wa Serikali Sunday Hyera na Edgar Bantulaki. Katika
shtaka la kwanza, mbele ya hakimu Agripina Kimaze anadaiwa Oktoba 15, saa 10:30
jioni alitenda kosa la kutishia kuua eneo la Mkambarani, Manispaa ya Morogoro.
Anadaiwa
katika shtaka hilo la jinai namba 226 la mwaka 2016, alitishia kumuua kwa
bastola askari namba 5057, Koplo Tuti Ndaga wa Kikosi cha Usalama Barabarani
Mkoa wa Morogoro, kinyume na kifungu namba 89 (1),(2),(a) cha Sheria ya Kanuni
ya Adhabu namba 16.
Katika shtaka la pili la ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani lenye makosa matano, ilidaiwa kuwa; kwanza, siku na muda huo eneo la Mbuyuni Mkambalani, mshtakiwa alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Prado lenye rangi ya kijivu bila kuwa na leseni.
Katika shtaka la pili la ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani lenye makosa matano, ilidaiwa kuwa; kwanza, siku na muda huo eneo la Mbuyuni Mkambalani, mshtakiwa alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Prado lenye rangi ya kijivu bila kuwa na leseni.
Pili,
ilidaiwa alikuwa akiendesha gari hilo ambalo halikuwa na bima; tatu, alikutwa
akiendesha kwa mwendo kasi; na nne, alikataa kupeleka gari Kituo cha Polisi cha
Kingoluwira kama alivyoamriwa na askari, WP namba 5392 Sajenti Anna.
Ilidaiwa
katika shtaka la tano kwamba, wakati akiendesha alisimamisha gari katikati ya
barabara kuu ya Morogoro-Dar es Salaam kwa uzembe, bila uangalifu wala
kuzingatia watumiaji wengine wa barabara. Mkurugenzi huyo alikana mashtaka yote
yanayomkabili.
Hakimu
Kimaze alitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa kwamba awe na mdhamini mmoja
kwa kila shtaka, yaani shtaka la jinai na la usalama barabarani lenye makosa
matano, wote wawe wakazi wa Morogoro na mmoja akitakiwa kuweka dhamana ya
Sh500,000 kwa kosa la kwanza na Sh1 milioni kwa kosa la pili.
Mshtakiwa alikidhi masharti ya dhamana na kuachiwa huru, huku gari likiendelea kushikiliwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Morogoro.
Mshtakiwa alikidhi masharti ya dhamana na kuachiwa huru, huku gari likiendelea kushikiliwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Morogoro.
Hakimu
Kimaze aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 31, usikilizwaji wa awali
utakapoanza baada ya upande wa mashtaka kudai upelelezi umekamilika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Afikishwa Mahakamani Kwa Kosa La Kumtishia Bastola Askari wa Usalama Barabarani (Trafiki) ”
Post a Comment