Saturday, November 12, 2016
BENKI YAOMBA MAHAKAMA IIZUIE TANESCO KUILIPIPA IPTL, YASTUKIA ESCROW
Do you like this story?
Benki ya Standard Chartered Limited ya Hong Kong (SCB-HK) imefungua
maombi Mahakama Kuu ikitaka, pamoja na mambo mengine, Shirika la Umeme
(Tanesco) lizuiwe kuilipa kampuni ya uzalishaji nishati hiyo ya Independent
Power Tanzania Limited (IPTL).
Badala yake,
SCB-HK inaomba malipo hayo yahifadhiwe mahakamani hapo hadi Tanesco itakapolipa
dola 148 milioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh320 bilioni) kwa benki hiyo
kama Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID)
ilivyoagiza mwezi Septemba, tofauti na ilivyokuwa wakati wa mgogoro wa Tanesco
na IPTL wakati fedha zilipowekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika
uamuzi wake uliotolewa Septemba 12, 2016, ICSID iliamuru Tanesco iilipe SCB-HK
dola 148.5 milioni, pamoja na riba ya asilimia 4, kwa kipindi cha miezi mitatu
kuanzia Septemba 30, 2015, hadi malipo yote yatakapokamilika.
Uamuzi wa
ICISD ulikuja takriban miaka mitatu baada ya Serikali kuidhinisha malipo ya
takriban Sh306 bilioni kutoka akaunti ya escrow iliyofunguliwa na Tanesco kwa
kushirikiana na IPTL kusubiria uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu mgogoro wa malipo
ya tozo ya uwekezaji.
Mwaka 2005
SCB-HK, ilinunua deni ambalo benki ya Danaharta ya Malaysia ilikuwa ikiidai
IPTL baada ya kampuni hiyo kukopa dola 101.7 milioni za Kimarekani ili kununua
mtambo wa ufuaji umeme wa Tegeta wenye uwezo wa kuzalisha megawati 100.
Lakini
wakati fedha hizo zilipotolewa, ililipwa kampuni ya Pan African Power Solutions
(PAP), jambo lililofanya SCB-HK kufungua kesi hiyo ICSID ikidai ndiyo iliyostahili
malipo hayo, kesi ambayo benki hiyo ilishinda.
Umuzi huo wa
ICSID umeshakubaliwa na kusajiliwa na Mahakama Kuu Tanzania kupitia maombi
namba 687, ya mwaka 2016, yaliyofunguliwa na SCB-HK, na hivyo unatambulika kama
uamuzi wa mahakama hiyo.
IPTL inafua umeme
ambao unauzwa kwa Tanesco.
Lakini
SCB-HK imewasilisha maombi kwa hati ya dharura ikiomba mahakama iizue Tenesco
kuendelea kuilipa PAP, ambayo inamiliki IPTL na badala yake pesa hizo ziwe
zinahifadhiwa mahakamani hapo hadi deni hilo litakapolipwa lote.
Benki hiyo
inaiomba mahakama isikilize upande mmoja bila Tanesco kuwepo na iamuru fedha za
malipo hayo ya uwekezaji yanayofanywa na Tanesco kwa PAP, ziwe zinalipwa
mahakamani hapo kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi hayo.
Kwa mujibu
wa hati ya dharura iliyoambatanishwa na maombi hayo, wakili wa SCB-HK, Gaspar
Nyika anataka maombi hayo yasikilizwe kwa dharura akidai kuwa benki hiyo ndiyo
ina haki na malipo hayo kulingana na uamuzi wa ICSID.
Pia anasema
kama malipo hayo hayatahifadhiwa mahakamani kusubiri uamuzi wa maombi hayo,
SCB-HK itaathirika kwa kupata hasara ambayo haiwezi kufidiwa.
Wakili Nyika
anadai kuwa benki hiyo ilipewa haki dhidi ya mali na shughuli zote IPTL, baada
ya kampuni hiyo kushindwa kurejesha mkopo iliouchukua kutoka benki ya Danaharta
ulionunuliwa na SCB-HK mwaka 2005.
Katika
uamuzi wake, ICSID ilieleza kuwa kwa mujibu wa Mkataba wa Mauziano ya Umeme
(PPA) baina ya benki hiyo na Tanesco,
SCB-HK ndiyo yenye uhalali wa kisheria wa shughuli zote za IPTL.
Hivyo
anasema fedha zilizolipwa kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow hazikuliondolea
Tanesco wajibu wake kwa SCB-HK kwa mujibu wa PPA na hivyo hayawezi kupunguzwa
kutoka katika kiasi inachodaiwa na benki hiyo. Pia ICSID ilisema kuwa malipo
yaliyolipwa kwa IPTL/PAP tangu Agosti 2013, hayondoi wajibu wa Tanesco kwa SCB-HK chini ya PPA na
hivyo hayawezi kupunguzwa katika deni la SCB-HK, chini ya PPA.
Pia ICSID
ilisema kuwa kuchotwa kwa pesa zilizokuwa kwenye Akaunti Maalumu ya Tegeta
Escrow ( na kampuni ya Pan Africa Power Solution PAP inayodai kununua hisa zote
za IPTL) hakukuiondolea benki hiyo haki katika kampuni hiyo ya IPTL.
Uamuzi wa
ICSID uliwasilishwa Mahakama Kuu Oktoba 11, 2016 ili usajiliwe kwa ajili ya
utekelezaji.
Hata hivyo
siku hiyohiyo, Tanesco ilifungua maombi namba 686, ya mwaka 2016, ikiomba
kusimamishwa kwa usajili na utekelezaji wa uamuzi huo, kusubiri usikilizwaji na
uamuzi wa maombi yake ya kusimamishwa
kwa utekelezaji wa uamuzi huo katika ICSID.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BENKI YAOMBA MAHAKAMA IIZUIE TANESCO KUILIPIPA IPTL, YASTUKIA ESCROW”
Post a Comment