Tuesday, November 15, 2016
MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU AOKOA MILIONI 33 KWA KUPANDA NDEGE YA ATCL KWENDA MWANZA
Do you like this story?
Katika
kuendelea kujenga dhana ya kubana matumizi ya fedha za serikali, Makamu wa
Rais, Samia Suluhu Hassan amesafiri kwa ndege ya abiria ya Kampuni ya Ndege
Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na kuokoa zaidi ya Sh
milioni 33.
Kabla ya kuanza safari hiyo jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais akizungumza na waandishi wa habari, alisema kwa kupanda ndege hiyo ameokoa fedha za serikali na kodi za wananchi.
Alisema
ameona ashirikiane na Watanzania kuonesha uzalendo kwa kutumia huduma ambazo
zinatolewa na serikali na kuwataka Watanzania wote kutumia ndege hizo.
“Ningepanda
ndege ya kukodi ningetumia shilingi milioni 40 kwa safari hii, lakini nikaona
hapana nikaamua mimi pamoja na msafara wangu tutumie ndege hii ya Shirika la
Ndege Tanzania ambapo tumetumia Shilingi milioni 7.6 pekee,” alisema Makamu wa Rais aliyeambatana na
watu 16 katika safari hiyo.
Makamu
wa Rais ambaye alipanda ndege hiyo pamoja na abiria wengine wa kawaida,
aliwataka viongozi wengine pia kufuata mfano huo kusafiri kwa kutumia ndege za
shirika hilo.
Alisema
ameona kwenye televisheni watu wakitoa maoni yao juu ya kampuni hiyo ya ndege
kuwa ni nzuri kwa sasa na yeye akaamua kusafiri na ndege hiyo.
“Niliona
kwenye televisheni watu wakitoa maoni mazuri tu juu ya shirika hili na mimi
nikaona nitumie nafasi hiyo,”
alifafanua Makamu wa Rais.
Hivi
karibuni, serikali imenunua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 na
kuzikabidhiwa kwa ATCL na zimeanza kufanya kazi katika mikoa mbalimbali nchini
huku zikiwa na gharama nafuu, lakini pia zikiwa na gharama nafuu ya uendeshaji.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ambaye alikuwepo
uwanjani akimsindikiza Makamu wa Rais, alisema Watanzania waelewe kwa sasa
kampuni hiyo iko kwa ajili ya kufanya biashara.
Alimpongeza
Makamu wa Rais kwa kuonesha ushirikiano mkubwa na pia uzalendo kwa kusafiri na
ndege ya ATCL, kwani angeweza kutumia ndege nyingine yoyote.
“Leo
hii kwa kutumia ndege ya Tanzania yeye pamoja na wasaidizi wake ni jambo jema
sana alilolifanya na pia ni jambo la kizalendo tunampongeza sana, kwani
angeweza kutumia ndege nyingine yoyote anayoitaka,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema
ndege za ATCL gharama zake ni nafuu na pia huduma zao zimeboreshwa zaidi, na
kwamba ifikapo mwaka 2018 serikali itanunua ndege nyingine moja na pia mwaka
2019 inatarajia kununua ndege nyingine.
Mkurugenzi
Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema kampuni hiyo inaboresha huduma zake
ambako kwa sasa wanaboresha huduma za mtandaoni kwa ajili ya watu kushika
nafasi ya safari na hata kulipia kupitia mitandao ya simu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU AOKOA MILIONI 33 KWA KUPANDA NDEGE YA ATCL KWENDA MWANZA”
Post a Comment