Thursday, February 23, 2017
ZLATAN IBRAHIMOVIC;MAMBO 14 USIYOFAHAMU KUHUSU YEYE
Do you like this story?
Mwaka
2014, katika mahojiano na gazeti la The Guardian, Ibrahimovic alielezea
kwamba anakumbuka alipokuwa mtoto baba yake alitoa akiba yote ya pesa
alizokuwa nazo wakaenda dukani ili akamnunulie kitanda, baada ya kununua
kitanda hicho wakajikuta hawana pesa za kulipia usafiri wa kukipeleka
nyumbani, kwahiyo ikawabidi kukibeba wao wenyewe!
“Tulikibeba mimi na baba mpaka nyumbani. Nilifurahi tulivyokibeba.
Kuna kipindi alitoa mshahara wake wote ili niweze kwenda kwenye kambi ya
mazoezi. Alijua akinipa hataweza kulipa kodi ya nyumba, lakini alinipa
pesa hiyo ili niende kambini.”
Yafuatayo ni mambo 14 ambayo huyajui kuhusu Zlatan Ibrahimovic a.k.a. Ibracadabra:
14. Akiwa na miaka 10 aliingia uwanjani kutoka benchi na kufunga magoli 8!
Akiwa anachezea klabu yake ya mtaani ya FBK Balkan akiwa umri wa
miaka 10, Zlatan alichelewa kufika uwanjani kwenye mechi kwakuwa alikuwa
anaishi mbali na alikuwa akienda uwanjani kwa baiskeli. Aliingizwa
uwanjani kipindi cha pili wakati timu yake ipo nyuma kwa kufungwa magoli
5-0. Ibrahimovic akabadili matokeo ya mchezo huo kichwa chini miguu juu
baada ya kufunga magoli 8 – ndio, magoli 8, yote katika kipindi cha
pili tu, na kufanya washinde mchezo huo kwa magoli 8-5. Hapo ndipo jina
la utani “The Zlatan” lilipozaliwa rasmi na dunia nzima ikaanza
kufatilia kipaji cha hali ya juu cha bwana mdogo huyu.
13. Hataki kufanyiwa majaribio kabla ya kumnunua
Kwenye mahojiano aliwahi kuulizwa kwanini hakusajiliwa na Arsene
Wenger kuichezea klabu ya Arsenal alipokuwa kijana, jibu lake lilikuwa
ni kama ifuatavyo; “Zlatan hafanyiwi majaribio.” – alisema alipoulizwa
kuhusu Wenger alipomtaka ujanani kwake.
“Ukininunua mimi, ujue kuwa unanunua gari aina ya Ferrari. Ukitaka
kuendesha Ferrari unajaza petroli kwenye tenki, unatafuta barabara ya
lami ilipo na unakanyaga mafuta mpaka mwisho. Guardiola alinijaza dizeli
badala ya petroli, halafu akanipitisha barabara ya vumbi. Alitakiwa
kununua Fiat, sio Ferrari.” – alisema alipoulizwa kuhusu uhusiano wake
mbovu na kocha Pep Guardiola, kipindi hicho Jose Mourinho alikuwa
msaidizi wa Pep Guardiola.
12. Mfungaji bora wa timu ya Taifa ya Sweden
Zlatan Ibrahimovic alizaliwa nchini Sweden, baba yake ni raia wa
Bosnian na mama raia wa Croatia, ikimaanisha angeweza kuchagua kuchezea
timu yoyote ya Taifa kati ya hizo mbili kwenye mashindano ya kimataifa.
Alichagua Sweden kwa sababu ndipo alipozaliwa na kukua.
Yawezekana huo ulikuwa mbovu kwakuwa nchi hiyo imefuzu mara mbili tu
katika mashindano matano ya mwisho ya kombe la dunia, lakini hawezi
kubebeshwa lawama kwa hilo. Amejaribu kwa nguvu zake zote kuibeba timu
yake ya Taifa! Yeye ndiye mfungaji bora wa timu hiyo akiwa na magoli 62
kwenye timu ya Taifa kabla ya kustaafu.
11. Jina lake limeingizwa kwenye Kamusi nchini Sweden
Zlatan ni shujaa wa nchi ya Sweden kiasi kwamba jina lake limeongezwa
kwenye kamusi inayotumia lugha ya nchi hiyo! Mwaka 2012, Baraza la
Lugha ya Kiswidi lilitambua rasmi neno ‘Zlatanera’ litumike rasmi katika
lugha yao. Neno hili linatokana na jina la mchezaji huyo.
Neno ‘Zlatanera’ linamaanisha kumiliki au kufanya jambo kwa ufundi au uwezo wa hali ya juu sana!
10. Mgahawa nchini Ufaransa una baga (burger) yenye jina lake
Ibrahimovic alipata mashabiki wengi nchini Ufaransa hasa baada ya
kuhamia klabu ya PSG, na walikuwa wengi kiasi cha kufanya mgahawa mmoja
nchini humo kuwa na aina maalumu ya baga yenye jina la mchezaji huyo.
Mgahawa huo unaoitwa Doddy’s, upo katika mitaa ya Boulogne-Billancourt.
“Le Zlatan” ndio jina la baga hiyo na mmiliki wa mgahawa anasema kuwa
ndiyo “inayopendwa zaidi” na wateja wake kama ambavyo Ibra anapendwa na
mashabiki zake.
9. Anapenda filamu ya Scarface
Zlatan anasema kuwa filamu anayoipenda zaidi ni Scarface na huwa
anaitazama mara mbili au tatu kila mwaka. Pia ameshawahi kutangaza kuwa
kama akitaka kumualika mtu yeyote yule ili ale naye chakula cha jioni,
basi mtu huyo lazima atakuwa Al Pacino, Muigizaji Mkuu katika filamu
hiyo ya Scarface.
Kama kuna muigizaji atataka atengeneze filamu kuhusu maisha ya Ibra,
basi Ibra mwenyewe atamchagua Pacino kwakuwa anasema ndio mtu pekee
atayeweza kuigiza nafasi yake vizuri.
8. Uwanja wa mchangani aliojifunzia soka ulikarabatiwa kwa heshima yake
Ingawa yaweza kuonekana kwamba muda wote anafanya mambo kwa ajili ya
sifa, Ibrahimovic hasahau alipotoka. Alipokuwa mtoto alikuwa akijifunza
soka katika uwanja ambao awali ilikuwa bustani ya mama yake. Baada ya
kuwa mchezaji wa kulipwa, mwaka 2007 Zlatan akidhaminiwa na kampuni ya
vifaa vya michezo ya Nike waliutengeneza upya uwanja. Uwanja huo ambao
kwa sasa una uzio umepewa jina la “Uwanja wa Zlatan”, na utawezesha
kizazi kipya kujifunza mchezo wa soka katika mazingira bora zaidi ya
yale aliyojifunzia mcheza soka huyo wa kimataifa alipokuwa mtoto. Uwanja
huu una ujumbe usomekao: Hapa ndipo ulipo moyo wangu. Hapa ndipo ilipo historia yangu. Hapa ndipo ulipoanzia mchezo wangu. Upeleke mbali, Zlatan.”
7. Kuna sanamu lake kwenye makumbusho ya jijini Paris
Zlatan amekuwa ‘akitukuzwa’ katika makumbusho ya Musée Grévin jijini
Paris, Ufaransa kwa kuwa na sanamu lake. Sanamu hili linalomuonesha
anashangilia kwa kuinua mikono yote ikielekea mawinguni (aina ya
ushangiliaji anayoipenda zaidi). Katika makumbusho hii mchezaji mwengine
ambaye si Mfaransa kuwekewa sanamu ni Pele wa Brazil, kwahiyo amepewa
heshima ya kipekee sana. Hii inaonesha ni kwa jinsi gani amekuwa na
mchango mkubwa kwa jiji la Paris na kwa nchi ya Ufaransa toka ajiunge na
klabu ya PSG mwaka 2012.
6. Aliwapa zawadi wachezaji wenzake wa PSG toleo maalumu la ‘Xbox One’
Muda mfupi baada ya kushindwa kufuzu kwenda mashindano ya Kombe la
Dunia, Zlatan aliwashangaza wachezaji wenzake wa PSG kwa kuwapa zawadi
ya kifaa cha michezo ya video cha Xbox One (toleo maalumu), kila kimoja
kikiwa na jina la mchezaji husika na namba ya jezi yake – bila kusahau
sahihi ya Zlatan. Ibrahimovic ni balozi pekee wa vifaa vya Xbox One
nchini Ufaransa, ikimruhusu kuwapa wachezaji wenzake zawadi hiyo ya
kipekee aliyoibuni.
5. Ni mchezaji pekee kufunga kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa na timu sita tofauti
Zlatan amedhihirisha kuwa ni mshambuliaji wa kiwango cha kipekee bila
kujalisha jezi aliyoivaa kwa kufunga katika mashindano makubwa zaidi
Barani Ulaya katika ngazi ya vilabu akiwa na timu sita tofauti. Hili
linaashiria mambo mawili, kwanza yeye ni mfungaji wa kiwango cha juu
kabisa ambaye anaweza kukaa chini ya walimu tofauti, pia inaonesha kuwa
timu zote za juu katika ligi za Ulaya zinamuhitaji. Katika Klabu Bingwa,
amefunga magoli akiwa na klabu za Ajax, Juventus, Inter Milan,
Barcelona, AC Milan na PSG. Ingawa amezifungia magoli mazuri sana,
lakini mpaka sasa bado hajalibeba kombe hilo.
4. Alitabiri hatma ya maisha yake akiwa utotoni
Alipokuwa na miaka 16, Zlatan akijibu mtihani wake wa somo la
Kiingereza, katika swali lililoulizwa: “Utakuwa nani baada ya miaka
mitano?.”
Alichokiandika Zlatan kujibu swali hilo ni kwamba “nitakuwa mchezaji
wa kulipwa wa mpira wa miguu nchini Italia, nitalipwa pesa nyingi sana,
nitakuwa namiliki nyumba ya kifahari karibu na bahari na nitakuwa tajiri
mkubwa sana.”
Haya aliyajibu akiwa na miaka 16!
3. Alikuwa mwizi wa baiskeli utotoni
Zlatan amekulia katika sehemu ya watu maskini mjini Malmo, Sweden na
mara nyingi alikuwa akiiba baiskeli za watu na kuendesha kilomita 5
kwenda na kurudi mazoezini.
Alipokuwa mdogo, alikuwa na baiskeli aliyokuwa anaipenda sana lakini
ikaibwa. Kuanzia hapo na yeye akawa mwizi wa baiskeli kulipiza kisasi …
Alipokuwa klabu ya Malmo, Zlatan alienda mazoezini na baiskeli ambayo
aliiba, alipomaliza mazoezi akakuta imeibwa. Zlatan akaamua kuiba
baiskeli nyingine na kurudi nayo nyumbani.
Habari zilizopo ni kwamba alishawahi kuiba hadi baiskeli ya Meneja wa
timu yake kipindi fulani. Ilibidi wachezaji waliokuwa wanachezea timu
ya vijana waitwe kwenye kikao na ndipo Zlatan alipopewa somo refu baada
ya kugundulika yeye ndiye aliyeiba baiskeli hiyo. Zlatan alisema sababu
ilikuwa ni kuhitaji usafiri kwakuwa uwanja wa mazoezi ulikuwa mbali.
2. Ronaldo de Lima ndio shujaa wa Zlatan
Ibrahimovic amekuwa akimtukuza ‘The Phenomenon’ Ronaldo Luis Masouza
de Lima, mshambuliaji wa zamani raia wa Brazil, na mara zote huwa
anamuelezea kama mchezaji bora zaidi “kwa wakati wowote”
Ibra alihamia klabu ya Inter Milan mwaka 2006 akifuata nyayo za
shujaa wake huyo. Alipokuwa klabu ya Inter ndipo alikutana na bosi wa
sasa wa Man United, Jose Mourinho.
1. Ana mikanda miwili ya rangi nyeusi kwenye mchezo wa kupigana aina ya Taekwondo
Kwa aina ya tabia na uchezaji wake, Ibrahimovic huwa anajikuta kwenye
mabishano na ugomvi kati yake na wachezaji wa timu pinzani. Huyu ni
mchezaji ambaye hata wewe usingetaka awe mpinzani wako sehemu yoyote ile
kwakuwa ana uwezo wa kupigana kama ukimshinda kwenye kubishana. Uwezo
wake mkubwa wa kupigana ndio unaomuwezesha kuruka mateke ya juu ingawa
ana umbile kubwa.
Kuna vitu viwili ambavyo Zlatan anavipenda kupita kiasi: kwanza
kufunga magoli ya ajabu ya tikitaka yanayozidi kimo cha mtu, na pili
kuwapiga mateke ya kichwa wachezaji wenzake kama masihara wakiwa
mazoezini.
Zlatan ni mtaalamu wa kupigana, ana mkanda mweusi wa mchezo wa
kupigana aina ya Taekwondo ambao hutumia zaidi mateke alioupata nchini
Sweden akiwa na umri wa miaka 17 mjini Malmo, pengine ndio sababu
anapenda sana kuwapiga wachezaji wenzake mateke ya kichwa wawapo
mazoezini.
Mwaka 2010 akiwa anachezea klabu ya AC Milan ya Italia, alipewa
mkanda mweusi wa heshima na Shirikisho la Mchezo wa Taekwondo nchini
humo. Aliwahi kusema kuwa kama asingekuwa mcheza soka, basi angekuwa
mpiganaji wa kimataifa katika mchezo huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ZLATAN IBRAHIMOVIC;MAMBO 14 USIYOFAHAMU KUHUSU YEYE”
Post a Comment