Thursday, March 23, 2017

MWANAFUNZI WA DARASA LA 3 YUKO HOI KWA KUCHAPWA VIBOKO SHULENI


MWANAFUNZI wa darasa la tatu katika shule ya msingi ya St Joseph's Girls mjini Busia anauguza majereha kwenye makalio na mbavu baada ya kuadhibiwa kinyama.
Amedai amefanyiwa unyama huo mwalimu wake.

Akielezea Swahilihub yaliyomkumba Jumatano, mwanafunzi huyo wa kike mwenye umri wa miaka minane ambaye jina lake tumelibana kutokana na sababu za kiusalama, alisema alilazwa juu ya meza kabla ya mwalimu kuamuru wanafunzi wanne wamshike miguu na mikono kisha akaanza kumcharaza viboko na kusababisha majereha.
Vilevile aliongeza mwanafunzi huyo kutoka mtaa wa Marachi alifichua kuwa sababu ya kupokezwa adhabu hiyo iliyofanyika Alhamisi wiki iliyopita ni baada ya kuwasilisha kazi ya ziada ya somo husika akiwa amechelewa.
“Mwalimu alitupa kazi ya ziada na wenzagu darasani wakawa wepesi kumaliza kazi hiyo. Tulikutana na mwalimu yuyo huyo akiwa zamu na aliponiuliza 'unatoka wapi' nikamweleza 'natoka ofisini' kupeleka kitabu cha kazi ya ziada. Papo hapo akaniambia nilale chini na kuamuru wanafunzi wanne wanishike kabla ya yeye kuanza kunichapa. Siku hiyo nilihisi uchungu kwa makalio na mbavu ingawa nilijikaza hadi nyumbani na kuwaeleza wazazi,” amesema mwanafunzi huyo.
Naye, mamake mwanafunzi huyo BI Racheal Wambui ameelezea masikitiko ya mwanawe kuumizwa baada ya daktari katika hospitali ya rufaa ya Busia kubaini kiwango cha majereha.
“Mtoto alifika nyumbani akichechemea na nikamuuliza ni kwa nini. Aliniambia mwalimu alimwadhibu hadi kumuumiza. Nilichukua hatua na kumpeleka hospitalini na daktari akabaini kuwa alikuwa ameumizwa vibaya mbavuni na makalio baada ya kupiga picha za X-ray,” amesema Bi Wambui.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bi Florida Maliki amesema wamepokea habari kuhusu kisa hicho na wameanzisha uchunguzi kabla ya kuchukua hatua yoyote dhidi ya mwalimu huyo.
“Tumeanzisha uchunguzi kufuatia kisa hiki ili kutafuta ukweli kwa sababu tumepokea ripoti kinzani. Mtoto alisema alichapwa wakati wa mapumziko ya kwanza huku mwalimu naye akisema alikuwa katika darasa la nane wakati huo."
Bi Maliki aliongeza, “Walimu hawaruhusiwi kuwaadhibu watoto kwa viboko ila sheria inaturuhusu tu kuwapa wosia. Kulingana na mwalimu wake wa darasa, mwanafunzi alikuwa darasani Alhamisi na Ijumaa kabla ya malalamishi kuwasilishwa Jumatatu juma hili.”

0 Responses to “MWANAFUNZI WA DARASA LA 3 YUKO HOI KWA KUCHAPWA VIBOKO SHULENI”

Post a Comment

More to Read