Thursday, March 23, 2017

MWANAUME AIAMBIA MAHAKAMA HAWEZI ACHA KUVUTA BANGI


MWANAMUME aliyeambia mahakama kwamba hawezi kuacha kuvuta bangi kwa sababu ya kazi anayofanya, Jumatano alifungwa jela miaka mitatu kwa kupatikana na kisu akiwa na nia ya kutenda uhalifu.
Alfred Geventi Timona alikiri kwamba alipatikana na kisu na misokoto 12 ya bangi alipokamatwa na maafisa wa usalama katika barabara ya Mbagathi mnamo Novemba 21, 2016.

Mahakama ilisema mshtakiwa hakuweza kueleza alinuia kufanya nini na kisu alichopatikana nacho siku hiyo.
“Mshtakiwa hakueleza kwa nini alikuwa na kisu usiku. Kwa sababu hii mahakama imeridhika kwamba alinuia kutenda uhalifu alivyoshtakiwa,” alisema Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Kibera Elizabeth Juma.
Maafisa wa urekebishaji wa tabia walisema kwenye ripoti kwamba mshtakiwa hakufaa kupewa kifungo cha nje kwa sababu alikataa kufichua habari muhimu kuhusu familia na maisha yake.
Kuzoa takataka
Ripoti ilisema kwamba Geventi alikiri kwamba alikuwa mraibu wa bangi kwa sababu anafanya kazi ya kuzoa taka mtaani Kibera.
“Ninapendekeza kwamba mshtakiwa hafai kifungo cha nje kwa sababu hakueleza anakoishi na hakufichua waliko jamaa zake,” ilisema ripoti iliyoandikwa na afisa wa urekebishaji wa tabia wilaya ya Kibra, Ann Mungai.
Bi Juma alimtoza faini ya Sh20,000 kwa shtaka hilo na akamfunga jela miaka mitatu kwa kupatikana na kisu akijiandaa kutenda uhalifu.

0 Responses to “MWANAUME AIAMBIA MAHAKAMA HAWEZI ACHA KUVUTA BANGI”

Post a Comment

More to Read