Wednesday, March 22, 2017

ZIARA YA WAZIRI MAKAMBA MIKOANI, FAHAMU KISIWA KILICHOTOWEKA SABABU YA MAJI YA BAHARI KUONGEZEKA




Taarifa ya siku ya Pili ya ziara ya mahsusi ya kimazingira ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe January Makamba kutembelea mikoa 6 yenye lengo la kukagua shughuli za uhifadhi mazingira, usimamiaji wa sheria za mazingira pamoja kutoa elimu ya mazingira na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.

Katika siku ya pili ya ziara Waziri Makamba ametembelea Hifadhi ya Taifa ya Saadani ambayo ni hifadhi pekee  nchini  Tanzania  na  Afrika  Mashariki yenye  fukwe za bahari  na inayotazamana na Bahari  ya Hindi na hifadhi pekee  ambapo  fukwe za bahari  zake  zinakutana  na uoto wa asili  wa nchi kavu.

Waziri Makamba amepokea taarifa ya kimazingira ya hifadhi ya Saadani iliyoainisha changamoto kadha wa kadha za kimazingira zikiwemo mgogoro wa mipaka, uingizwaji holela wa mifugo katika eneo la hifadhi, uwepo wa njia nyingi za umma ndani ya hifadhi pamoja na mabadiliko ya uoto wa asili yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi yanayopelekea sehemu za hifadhi kutoka kati unto wa nyika kwenda vichaka jambo linaloathiri ekolojia.

Kabla ya ya kufanya majumuisho ya ziara ya mkoa wa Pwani Waziri Makamba ametembelea na kukagua shughuli za uzalishaji chumvi zinazofanywa na kiwanda kilichopo ndani ya hifadhi hiyo kiitwacho Sea Salt Limited kukagua shughuli za uzalishaji chumvi katika kiwanda hicho na kutambua namna gani zinavyoathiri mazingira.

Katika Majumuisho hayo Waziri Makamba amesisitiza kushughulikiwa kwa suala la uchimbaji mchanga katika eneo la kingo za Mto Mpiji ambapo ameainisha kuwa serikali inaandaa mwongozo na itatoa waraka kwa Serikali za Mitaa utakaosimamia shughuli zote za uchimbaji mchanga katika kingo za mito nchini kuanzia utoaji kibali cha uchimbaji mpaka usafirishaji ili kuhakikisha hali ya mito na vyanzo vya maji inakuwa ni ya kuridhisha wakati wote.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Alhaji Majid Mwanga amemshukuru Waziri Makamba kwa ziara yake katika Halmashauri mbili za Wilaya ya Bagamoyo na kuahidi kuhakikisha anasimamia utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa lakini hasa akimshukuru Waziri Makamba kwa mchango wa mifuko Mia Moja ya Sementi aliyoitoa kuchangia ujenzi wa Shule ya Msingi Kibindu.

Waziri Makamba amesema kufuatia changamoto kubwa ya maji wilayani Bagamoyo serikali itatoa Visima 17 virefu vya maji kwaajili ya wananchi lakini pia itatengeneza makinga maji “Water harvest” katika shule 5 hivyo ameutaka uongozi wa wilaya kutengeneza orodha kuona sehemu ambazo miradi hii itaelekezwa ambapo itafikia wananchi wengi iwezekanavyo katika wilaya nzima.

Baada ya majumuisho ya ziara katika mkoa waPwani Waziri Makamba alianza ziara katika mkoa wa Tanga ambapo amefika katika kijiji cha Buyuni kilichopo karibu sana na Bahari ya Hindi eneo ambalo ni hatarishi sana endapo patatokea machafuko baharini. Waziri amepokea pendekezo kuwahamishia wananchi wa kijiji hicho katika sehemu nyingine akiahidi mamlaka husika kukaa na kufanyia kazi mapendekezo hayo kwa wakati.

Waziri Makamba pia amefika katika Wilaya ya Pangani ambapo amekagua ujenzi wa moja kati ya miradi mikubwa ya kimazingira inayosimamiwa na Wizara yake unaolenga kudhibiti kuinuka kwa kina cha bahari kunakosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi yanayopelekea kuinuka kwa kina cha bahari hali inayopelekea kuliwa kwa eneo la nchi kavu.

“Tuna fahari mradi huu unaenda kwa kasi kubwa, kama mnavyoona na miradi yote hiii tunayoisimamia tutaizindua katika wiki chache zijazo na hatuna shaka kabisa tutauoko mji wa Pangani. Katika nchi yetu Pangani ni kielelezo cha mabadiliko ya tabia nchi, tulikuwa na kisiwa hapa kinaitwa Maziwe na watu walikuwa wakifanya shughuli zao lakini sasa hivi kimepotea kabisa kwasababu bahari imeinuka”. Alisema Waziri Makamba

Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi Zainabu Abadallah amemshukuru Waziri Makamba kwa kusimamia mradi huo aliouita wa kiukombozi kwa wananchi wa Pangani ambapo amesema mradi huo hauna faida za kimazingira pekee bali pia una faida mbalimbali za kiuchumi kwani vijana wengi wa Pangani wamepata ajira katika kushiriki ujenzi wa mradi huo.
Waziri Makamba anatarajiwa kutembelea wilaya nne za mkoa wa Tanga kabla ya kuelekea mkoani Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida na baadae Dodoma

0 Responses to “ ZIARA YA WAZIRI MAKAMBA MIKOANI, FAHAMU KISIWA KILICHOTOWEKA SABABU YA MAJI YA BAHARI KUONGEZEKA”

Post a Comment

More to Read