Monday, March 27, 2017

WALICHOKUTA KAMATI YA BUNGE YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA MKOANI NJOMBE


Kamati ya kudumu ya bunge Utawala na Serikali za Mitaa imetembelea mkoani Njombe na kukagua baadhi ya miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF,TAMISEMI, Mfuko wa Rais wa Kujitegemea na MKURABITA na kuridhishwa na mchango wa taasisi hizo katika kupiga vita umasikini kwa kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Wakiwa mkoani humo,wajumbe wa Kamati hiyo walikutana na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaotekelezwa na TASAF ambapo licha ya kuvutiwa na hatua ya kujiongezea kipato kutokana na ruzuku kwa kuanzisha miradi midogo midogo, lakini pia walipongeza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya na lishe katika kaya za walengwa hao.

Aidha wajumbe wa kamati hiyo ambao waliongozana na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki pia wamepongeza hatua ya TASAF ya kupunguza tatizo la makazi ya walimu kwa kujenga nyumba katika kijiji cha Uwemba nje kidogo ya mji wa Njombe.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe.Kairuki amesema serikali itaendelea kuweka mkazo katika miradi inayolenga kuwapunguzia wananchi adha ya umasikini hivyo akataka wananchi kuitumia fursa hiyo vizuri ili waweze kuboresha maisha yao.Waziri huyo alionyesha kuridhika na baadhi ya wananchi mkoani Njombe kwa kutumia fursa zilizowekwa na serikali kuendesha shughuli za kiuchumi kikiwemo kilimo,ufugaji ,biashara na uanzishaji wa vikundi vya kuweka akiba.

Kwa Upande wa MKURABITA,Wajumbe wa Kamati hiyo walipata ushuhuda kutoka kwa baadhi ya wananchi ambao wamepata mikopo kwa kutumia hati za ardhi iliyopimwa chini ya Mpango huo ambao baadhi yao wameweza kupanua biashara zao baada ya kukopa fedha kwa wastani wa shilingi milioni 80 na kurejesha mikopo hiyo kwa wakati 

Kwa upande wake Mwenyekiti aliyeongoza wajumbe hao,Mhe. Venance Mwamoto alitoa wito kwa wataalamu walioko kwenye maeneo ya wananchi kutumia muda wao mwingi kuwapatia elimu na mafunzo yatakayowawezesha kuboresha miradi wanayoianzisha ili iwe endelevu na yenye kuleta tija.

Hata hivyo wanufaika wa mikopo kutoka taasisi za fedha walionyesha kilio chao kutokana na riba kubwa wanayotozwa jambo ambalo wamedai kuwa linaathiri maendeleo ya biashara zao na kufifisha nia ya kuendelea kukopa .Zifuatazo ni picha za ziara hiyo ya kamati ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa mkoani Njombe.
 Wajumbe wa kamati ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakikagua ujenzi wa nyumba ya Walimu inayojengwa na TASAF katika kijiji cha Ulembwe nje kidogo ya mji wa Njombe. 
 Wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali Mitaa wakipata maelezo ya mradi wa ujenzi wa nyumba ya Walimu katika kijiji cha Ulembwe inayojengwa TASAF ikiwa ni jitihada za serikali za kutatua tatizo la makazi kwa walimu.

 Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa , wakisalimiana na walengwa ya TASAF katika kijiji cha Ulembwe mkoani Njombe katika ziara ya kamati hiyo kukagua miradi ya TASAF,MKURABITA,TAMISEMI na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea.
 Mkuu wa mkoa wa Njombe ,Christopher ole Sendeka (watatu  kulia), baadhi ya wabunge na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga (aliyevaa Kaunda suti nyeusi ) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika kijiji cha Uwemba mkoani Njombe.

 Baadhi ya walengwa wa TASAF katika wa kijiji cha Ulembwe ,nje kidogo ya mji wa Njombe wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge waliofanya ziara kijijini hapo .Wakiwa kijijini hapo ule usemi wa mgeni njoo mwenyeji apone ulidhihirika baada ya Waziri Kairuki kuahidi kumsomesha mmoja wa watoto kutoka kaya ya mlengwa hadi kidato cha nne. 
 Wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya utawala na serikali za mitaa wakipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wananchi walionufaika na fedha kutoka mfuko wa Rais wa kujitegemea katika mji wa Makambako mkoani Njombe ambaye anaendesha kilimo cha viazi mviringo.
 Waziri Kairuki na Wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Utawala bora na Serikali za Mitaa wakiangalia bidhaa za ususi zinazofanywa na baadi ya wanawake kupitia kikundi chao kilichowezeshwa na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea mjini Njombe.
 Baadhi ya Wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya utawala na serikali za mitaa wakipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wanufaika wa Mfuko wa Rais wa kujitegemea mkoani Njombe aliyetumia fedha alizokopeshwa na mfuko huo kuanzisha mradi wa kufuga n’gombe.

 Waziri Kairuki wa kwanza kushoto akifuatiwa na mhe. Mwamoto,wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Njombe akiwemo mkuu wa mkoa huo Christopher Ole Sendeka ,nyuma yao ni baadhi ya wanufaika wa MKURABITA. 
 Waziri Kairuki aliyevaa gauni lenye rangi nyekundu na Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya utawala na serikali za mitaa mhe. Venance Mwamoto wakitoa nasaha kwa baadhi ya wanufaika wa MKURABITA mkoani Njombe.
 ‘’Karibuni tena Mkoani Njombe’’ndivyo wanavyoelekea kusema wenyeji kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa waliotembelea mkoa huo kukagua miradi ya TASAF,TAMISEMI ,MKURABITA na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea.
Waziri Angellah Kairuki watatu kutoka kushoto mstari wa mbele akiwa na Mhe.Magreth Sitta na Mhe.Ruth Mollel ambao ni wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge wa utawala na serikali za mitaa wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Ulembwe nje kidogo ya mji wa Njombe.

0 Responses to “WALICHOKUTA KAMATI YA BUNGE YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA MKOANI NJOMBE”

Post a Comment

More to Read