Friday, April 7, 2017
Serikali imefuta tozo katika mazao ya pamba, chai na kahawa
Do you like this story?
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali imefuta baadhi ya tozo katika mazao ya pamba, chai na kahawa
ambazo ni kero kwa wakulima ikiwemo ya sh. 450,000 iliyokuwa inatolewa
na kila kiwanda cha kuchambua pamba kwa ajili ya kuchangia mbio za
Mwenge.
Amesema tozo nyingine iliyofutwa kwa zao la pamba ni ada ya vikao vya
Halmashauri za Wilaya ambayo ni sh. 250,000, ambapo katika zao la chai
kodi ya moto na uokoaji imeondolewa na kwenye zao la kahawa, ada ya
leseni ya kusindika kahawa ya Dola za Marekani 250 imefutwa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 6, 2017) katika
hotuba yake ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya
mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge
kwa mwaka 2017/2018 Bungeni mjini Dodoma.
Amesema kufutwa kwa tozo hizo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali kwa
wakulima nchini ili kuwapunguza kodi, tozo na ada mbalimbali
zinazochangia kuwapunguzia faida.
“Serikali pia imeboresha mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuanzisha
utaratibu wa wazi wa ununuzi wa mazao kupitia minada na katika msimu wa
mwaka 2016/2017 kwenye zao la korosho, utaratibu huo umechangia kwa
kiasi kikubwa kuongezeka kwa bei ya korosho kwa kilo kutoka sh 1,200
hadi sh 3,800, bei ambayo haijawahi kufikiwa katika historia ya zao la
korosho nchini,” amesema.
Amesema mfumo huo wa stakabadhi ghalani na utaratibu wa minada
umeongeza ushindani na kuvutia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi
hususan nchi ya Vietnam na nchi nyingine kuja wenyewe kununua korosho
badala ya kutegemea soko la India pekee.
Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea na
uchambuzi wa kina wa kodi, tozo na ada zilizobaki katika sekta za
kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuziondoa au kuzipunguza ili
kumwezesha mkulima kunufaika zaidi na jasho lake na kuongeza mapato ya
Halmashauri.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Bunge lilipitisha Sheria ya
Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016, ambayo ni muhimu katika
kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika Sekta ya Habari nchini,
ambapo Kanuni za Sheria hiyo zimeandaliwa na tayari zimeanza kutumika.
“Natoa wito kwa wadau wa sekta ya habari kuzingatia sheria na kanuni
hizo ili kuimarisha weledi katika tasnia ya habari. Aidha, nashauri
wadau wa habari kujikita zaidi katika kuandika na kutangaza habari za
masuala ya maendeleo na uchumi ili kuwasaidia wananchi kutekeleza azma
ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha
huduma za kijamii,” amesema.
Pia Waziri Mkuu amevikumbusha vituo vya televisheni kuweka wakalimani
wa lugha katika vituo vyao. Amesema katika mwaka 2017/2018, Serikali
itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa
vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu shuleni na vifaa vya
kufundishia.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kwamba Serikali imeendelea kutoa
huduma pamoja na kuongeza upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye
ulemavu na katika kutimiza azma hiyo, amewaagiza Wakuu wa Mikoa
kuhakikisha kuwa Kamati za Watu wenye Ulemavu zinaanzishwa katika ngazi
za Mikoa, Wilaya, Mitaa na Vijiji.
Pia Serikali imeanzisha kampeni za kupinga unyanyapaa na vitendo vya
kikatili dhidi ya watu wenye ualbino katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza,
Geita, Simiyu, Kagera, Tabora, Kigoma, Mara, Mbeya, Katavi na Rukwa na
kampeni hiyo itaendelea nchi nzima.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980, DODOMA ALHAMISI, APRILI 6, 2017.
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980, DODOMA ALHAMISI, APRILI 6, 2017.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “Serikali imefuta tozo katika mazao ya pamba, chai na kahawa”
Post a Comment