Friday, April 7, 2017
Serikali yaunganisha shule 417 kwenye mtandao wa intaneti
Do you like this story?
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Viettel ya Vietnam inatekeleza
mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano vijijini ambao
umefanikisha kuweka miundombinu ya mtandao wa intaneti kwenye shule 417
hapa nchini.
Amesema mradi huo ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu
kuanzia 2015-2017, umewezesha pia ofisi za Halmashauri za Wilaya 123,
Hospitali za Wilaya 74, Vituo vya Polisi vya Wilaya 131 na Ofisi za
Posta 68 kufikiwa na mtandao huo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 6, 2017) Bungeni
mjini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa
kazi za Serikali kwa mwaka 2016/2017 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa
mwaka 2017/2018 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya
Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake ukiwemo Mfuko wa Bunge
kwa mwaka 2017/2018
Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2016/2017, baadhi ya kazi
zilizofanyika kwenye sekta ya mawasiliano ni pamoja na ujenzi wa Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano; Mradi wa Anuani za Makazi na Postikodi; na
kuanzisha huduma ya kituo cha Jamii Centre kitakachorahisisha utoaji wa
huduma muhimu katika kituo kimoja. Huduma hizo ni kulipa pensheni,
ankara na huduma za kibenki.
“Sekta ya mawasiliano inatekeleza Programu ya Miundombinu ya Kikanda
ambayo inahusisha Mradi wa Shule Mtandao (e-school), Mradi wa Video
Conference ambao unahusisha ununuzi, usimikaji na ufungaji wa vifaa vya
TEHAMA katika mikoa 26 na taasisi za Serikali,” amesema.
Amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa kituo cha kuhifadhi taarifa
na mifumo ya Serikali (Government Data Centre) ambacho lengo lake ni
kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa unaoenda sambamba na uhakika wa
upatikanaji wa taarifa za Serikali katika kutekeleza majukumu yake ya
kila siku.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa viwanda, Waziri Mkuu amesema Serikali
inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati
na vikubwa ili kujenga uchumi wa viwanda, na kwamba inatoa kipaumbele
kwenye viwanda vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa nchini,
vinavyotoa ajira kwa watu wengi na vinavyozalisha bidhaa zenye soko hapa
nchini na nje ya nchi.
“Katika kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye uchumi
wa viwanda, Serikali inahamasisha zaidi sekta binafsi ya hapa nchini
pamoja na mashirika ya umma kujenga viwanda. Jitihada hizo zimewezesha
mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF, PPF, LAPF, GEPF, PSPF na NHIF kuanza
kufufua, kuendeleza na kujenga viwanda vipya vipatavyo 27 katika maeneo
mbalimbali nchini,” amesisitiza.
Ameyataka mashirika ya umma yahakikishe kwamba mipango yao inaendana
na utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ambao dhima yake
ni kujenga uchumi wa viwanda.
Akizungumzia kuhusu juhudi za Serikali kupambana na rushwa, Waziri
Mkuu amesema Serikali inapambana na rushwa kwa nguvu zake zote na haina
mzaha wala uvumilivu na vitendo vya rushwa.
“Hatua zilizochukuliwa kupambana na rushwa tangu Serikali ya Awamu ya
Tano iingie madarakani Novemba, 2015 zimetambuliwa na mashirika ya
Kimataifa yanayojishughulisha na tafiti kuhusu masuala ya rushwa
duniani. Taarifa ya Shirika la Transparency International kwenye utafiti
wake kuhusu mtazamo wa rushwa mwaka 2016, imeonesha kuwa viwango vya
rushwa vinaendelea kupungua hapa nchini,” amesema.
Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha
2016/2017, Serikali iliweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 9.75
kutokana na operesheni zilizofanywa na TAKUKURU,
“TAKUKURU imefanya uchunguzi wa majalada 306 ya tuhuma za rushwa na
kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini kuendelea na mashtaka
kwa majalada 104. Katika kipindi hicho, TAKUKURU iliendesha kesi 674
zikiwemo kesi mpya 182, ambapo katika kesi 97 watuhumiwa walipatikana na
hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini. Kesi 407 zinaendelea
kusikilizwa mahakamani,” amesema.
Amesema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaendelea na mapambano
dhidi ya rushwa hususan katika eneo la ukusanyaji mapato ya Serikali,
kudhibiti matumizi ya fedha za umma, malipo hewa, matumizi mabaya ya
fedha za ushirika na kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya
maendeleo.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imefungua balozi mpya
sita katika nchi za Algeria, Israel, Korea Kusini, Sudan, Qatar na
Uturuki. Amesema Balozi hizo zina kazi ya kuendeleza juhudi za
kuitangaza Tanzania kama nchi yenye vivutio vingi vya utalii na
rasilimali zinazoweza kutumika kuvuta uwekezaji kutoka mataifa hayo
ikizingatiwa utulivu na amani iliyopo nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA, ALHAMISI, APRILI 6, 2017.
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA, ALHAMISI, APRILI 6, 2017.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “Serikali yaunganisha shule 417 kwenye mtandao wa intaneti”
Post a Comment