Thursday, April 13, 2017

Simba yamponza Golikipa wa Mbao FC


Uongozi wa Mbao FC umebaini utovu wa nidhamu ulikithiri katika kikosi chao wakati wa mchezo dhidi ya Simba uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza mwanzoni mwa juma hili.

Afisa habari wa Mbao FC Crinstant Malinzi amesema baada ya kikao cha viongozi kilichoketi jana, wamebaini suala hilo na tayari wameanza kuchukua hatua za kinidhamu kwa kumsimamisha mlinda mlango wao Erick Ngwegwe.

“Kweli kikao kilichofanyika jana na leo kimefikia mwafaka wa kumsimamisha mchezaji golikipa wetu aliyedaka kwenye mechi dhidi ya Simba Erick Ngwegwe kwa muda usiojulikana kwa kile kinachoashiria kwa namna moja au nyingine kuwa ni upangaji wa matokeo ili kupisha uchunguzi wa kamati zinazohusika na mambo hayo na kutuletea taarifa kamili kws ajili ya kufanya maamuzi. Kwa hiyo kwa sasa Ngwegwe ameondolewa kambini wakati timu inajiandaa na mechi dhidi ya Tanzania Prisons siku ya Jumapili,” amesema Malinzi wakati akithibitisha kusimamishwa kwa Ngwegwe.

“Mwenyewe anasema ni makosa ya kimchezo, lakini kwa dondoo za awali tulizozipata tumeona kuna viashiria vya utovu wa nidhamu wa makusudi uliopelekea matokeo kuwa vile. Kwa hiyo kwakua tunaendelea na uchunguzi, tumeamua tumuondoe kabisa kambini ili tusiharibu uchunguzi wakati bado tunaendelea na maandalizi ya meche zetu.”

Tuhuma hizi zomemuangukia golikipa pekeake hakuna mchezaji mwingine tuliyembaini hadi sasa kutokana na uchunguzi wa awali tulioufanya. Ikithibitika rungu zito litamuangukia kutoka katika klabu ya Mbao lakini kama hatakuwa na hatia basi atarejeshwa kwenye klabu hapo baadae.”

“Kuna rushwa za aina nyingi, kuna kuipendelea timu bila kupewa chochote wala kushawishiwa lakini inawezekana mchezaji akawa na mapenzi na timu fulani na anataka ipate matokeo mazuri. Unapocheza na hizi timu zinakua na mambo mengi sana zinakua kama zimeuteka mpira wa Tanzania.”

“Hatujamfukuza tumemsimamisha kupisha uchunguzi ili tuweze kubaini nini kilifanyika, baada ya hapo tutatoa ripoti yetu.”

Ngwegwe anatuhumiwa kuifungisha timu yake (Mbao FC) wakati ikicheza na Simba na kupoteza kwa kufungwa magoli 3-2. Mbao FC ilifunga magoli yake mawili kipindi cha kwanza na iliongoza hadi dakika 82 na Simba kuanza kurudisha.

Golikipa huyo mrefu anahusishwa na kuchukua kitu kidogo ili kuipa Simba ushindi. Goli linalolalamikiwa zaidi ni lile ambalo alushindwa kuudhibiti mpira na kusababisha mshambuliaji wa Simba Frederick Blagnon kufunga kwa urahisi.

0 Responses to “Simba yamponza Golikipa wa Mbao FC ”

Post a Comment

More to Read