Sunday, April 16, 2017

Tahadhari waliyoichukua Wabunge waliotishiwa kutekwa


C9OF6ezXoAA66tI
Baada ya taarifa ya Mbunge wa Nzega Mjini kwa tiketi ya CCM, hussein Bashe kuwa kuna wabunge 11 ambao wako katika orodha ya watu awnaoweza kutekwa wakati wowote, imesababisha wanaotajwa kurekebisha mienedno yao kuepuka kunaswa huku wengine wakisema kuwa hawana hofu.
Kwa Bashe hali imekuwa tofauti kwa ni amesema kuwa amebadilisha mwenendo wake wa maisha kwa kutoa taarifa kila anakokwenda.
“Nimeanza utaratibu wa kutoa taarifa ya sehemu ninayokwenda. lakini vitisho haviwezi kuubadilisha mfumo wangu a maisha wala kubadilisha ninachokiamini”  alisema Bashe.
Bashe alisema kuwa lailazimika kuliongelea suala hilo bungeni kwani vitisho hivyo siyo dhidi yake pekee bali pia kwa wabunge wengine pamoja na watanzania kwa ujumla.
Mbunge huyo alisema Bungeni kuwa alitekwa na maofisa wa Usalama wa Taifa na kuongeza kuwa kuna wabunge ambao bado wanasakwa na maofisa hao.
Wabunge wanaodhaniwa kuwa ndiyo haswa wanasakwa ni pamoja na Aeshi Hilary- mb. Sumbawanga Mjini(CCM), Mwita waitara -Ukonga(CHADEMA), Tundu Lissu- Singida Mashariki(CHADEMA), Zitto Kabwe- Kigoma mjini(ACT) Mwigulu Nchemba waziri wa mambo ya ndani na Nape Nnauye aliyevuliwa uwaziri na kutishiwa kwa bastola alipotaka kufanya mkutano na waandishi wa habari katika hoteli ya Protea.
Vilevile Mbunge Aeshi naye alieleza woga aliokuwa nao na namna alivyoamua kubadilisha mtindo wake wa namna ya kuishi ambapo huwapigia simu watu wake wa karibu kuwaeleza anapokwenda baada ya kudai alitishiwa wazi wazi na kiongozi wa Serikali mkoani Dar es Salaam.
“Mwenzako tangu nitishiwe na yule kiongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, nimekuwa nikiishi kama popo na kila sehemu ninapoenda napiga simu kwa watu mbalimbali kuwaeleza sehemu nilipo. Hata kwenye simu yangu nimetegesha GPS kwa ajili ya wengine kujua eneo nilipo” alisema Aeshi
Mbunge wa jimbo la Ukonga, Waitara alisema kuwa yeye tokea atajwe kwenye orodha ya wanaotakiwa kutekwa amekuwa akiishi kwa hofu kubwa na maisha yake kuwa ya taharuki. Alifika mbali na kusema kuwa eneo wanamoviziwa wabunge hao ili watekwe ni katika geti la kutokea la ukumbi wa Bunge na kuiomba serikalli kulitazama suala hilo kwa umakini zaidi badala ya kulipuuzia tu.
“Maisha yang ni ya wasiwasi kwa sababu mtoa taarifa anasema hao watu wanaotaka kutukamata wapo. Wameelekezwa waje Dodoma na sehemu wanayotuvizia ni kwenye geti la kutokea bungeni.” alisema waitara
“Nimechukua hatua za ulinzi binafsi kwa namna ambayo siwezi kusema ni ulinzi upi, ila kwa sasa nimekuwa mwangalifu na sehemu ninazokwenda kutembea” aliongeza.
Kwa upande wa wabunge wengine hawakuonesha kutishika na suala hilo la utekwaji nyara lililoletwa bungeni na Bashe na kueleza kuwa hakuna kitu kama hicho na watu wapuuzie kwani i propaganda zinazolenga kuichafua nchi na kuwapa hofu wananchi wake.
Moja ya wabunge waliotajwa katika orodha na hawajaonyesha kushtushwa ni Zitto Kabwe ambaye alisema kuwa hiyo ni hali ya kupeana hofu ambayo ni lazima ipuuzwe kwani inaweza kuacha taharuki kwa wananchi.
“Nadhani ni mambo ya kupeana hofu tu. Kwanza, sijafanya lolote la kusababisha nitekwe, niteswe ama kupotezwa. Hivyo habari hizi nazidharau kwa sababu sioni sababu kwanini nitekwe” alisema Zitto
Zitto aliwasilisha hoja bungeni ya kutaka iundwe kamati teule ya kuchunguza matukio yote ya utekaji na wananchi kuteswa. Alisema kama kweli kuna watu wenye mpango wa kumteka, wajipange vizuri na wajiandae sana.
“Wanaweza kupanga kuniteka wakanitafuta wakakuta mti wa mrumba au bwawa la Karosho au ziwa Tanganyika. Wathubutu tu wataona” alisema Zitto
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba, ambaye pia alitajwa kama moja ya wabunge ambao wanaweza kutekwa muda wowote, yeye alieleza kuwa hana hofu yoyote ya kutekwa na anapenda kuwaambia wabunge wengine waliopata tishio la kutekwa wasiwe na hofu kwa kuwa jambo hilo halipo.
“Ngoja nikuambie, kwanza hakuna kitu kama hicho. Pili hakuna sababu ka,a hiyo na tatu nchi yetu haijafikia hatua kama hiyo. Nadhani ama hofu ya watu au watu wenye nia ya kutengeneza taharuki na kutaka kuchafua nchi yetu. Kwa maana hiyo mimi kama Waziri ninayeshughulikia masuala ya usalama wa raia kwa ujumla ninawaambia hakuna kitu kama hicho.” alisema Mwigulu

0 Responses to “Tahadhari waliyoichukua Wabunge waliotishiwa kutekwa”

Post a Comment

More to Read