Wednesday, May 3, 2017
UTAFITI: Mbegu za maboga zinavyosaidia nguvu za kiume kuliko supu ya pweza
Do you like this story?
Kwa mujibu wa madaktari mbalimbali, mbegu za
maboga zina kiwango kikubwa cha virutubishi vya vitamin na madini na
hivyo kusaidia katika kuupa mwili nguvu na kuukinga dhidi ya maradhi
mbalimbali yakiwamo baadhi ya aina za saratani, kisukari, moyo na ini.
Imeelezwa na wataalamu kuwa kama ilivyo kwa
sifa ya mnofu wa pweza, mbegu za maboga pia zina sifa ya kuwa sawa na
kifurushi cha madini yanayomfaidisha mlaji kwa wakati mmoja, baadhi
yakiwa ni ya chuma, manganizi, maginizia, zinki na shaba. Walaji wa
mnofu wa pweza hunufaika pia kwa wingi wa virutubishi kama protini,
mafuta (fats) vitamin B12, selenium, madini ya chuma, shaba na vitamin
B6.
Imebainika kuwa viini lishe vilivyomo ndani ya
mbegu za maboga vina faida kubwa ikiwamo ya kuimarisha afya za uzazi
sababu inayochochea kuongeza kwa matumizi yake kiasi cha kutishia
umaarufu wa supu ya pweza.
“Kwa kweli mbegu za maboga sasa zimekuwa dili
kubwa mjini. Hapa katika Soko la Stereo (Temeke) huwa zinauzwa kuanzia
Sh. 10,000 katika ujazo wa chupa kubwa ya maji na watumiaji wake wengi
wanasifu kwamba zenyewe zina faida kubwa kwa watumiaji wakiwamo kina
baba wenye matatizo ya upungufu wa nguvu za kiume,” mfanyabiashara mmoja
wa maboga na matikiti maji katika soko la Stereo alisema.
Mbegu hizo za maboga huuzwa Sh. 3,000 kwa
vipimo vidogo vya chini ya nusu kilo katika Soko la Mwananyamala, jirani
na Kwa Kopa na pia katika baadhi ya maduka makubwa yakiwamo ya Tabata
Segerea huuzwa hadi Sh. 15,000 kwenye mfuko wa ujazo usiofikia kilo
moja.
Katika baadhi ya maeneo, wapo wafanyabiashara
wanaopita kwenye baa mbalimbali na kuwauzia wanywaji mbegu hizo kwa bei
ya wastani wa Sh. 2,500 kwa kikombe kidogo kama cha kahawa.
“Asiyejua anaweza kuona kuwa hizi tunaziuza
kwa bei ya juu (ya Sh. 2,500 kwa kikombe kidogo). Lakini ukweli ni
kwamba na sisi tunazinunua sokoni kwa bei kubwa sana siku hizi na
maandalizi yake yanachukua muda mrefu,” alisema mmoja wa wauzaji wa
mbegu hizo zilizokaangwa vizuri na kuwekwa chumvi kwa mbali,
akijitambulisha kwa jina moja la Grace.
“Ila kinachonipa moyo binafsi ni kwamba wateja
wamekuwa wakiongezeka sana na wengi wanazifurahia kwa ladha yake nzuri
na pia kuwasaidia kiafya…wanaume ndiyo wanazinunua sana huku wakisema
kwamba zina faida kubwa kwao kama ilivyo supu ya pweza,” aliongeza
Grace.
Sajjad Fazel, Daktari wa Tiba na Dawa katika
Hospitali ya Sanitas ya Mikocheni jijini Dar es Salam, alisema kuwa
maboga na mbegu zake vina faida nyingi mwilini na kwamba, kufahamika
zaidi kwa taarifa zake katika siku za hivi karibuni kunaweza kuwa chanzo
cha kuongezeka kwa watumiaji wake kila uchao.
Dk. Fazel alisema baadhi ya faida za mbegu na
pia maboga yenyewe kwa walaji ni pamoja na kuwaepusha na uzito wa mwili
kupita kiasi, kuwaongezea kiwango cha uoni wa macho kutokana na kuwa na
viini viitwavyo ‘beta-carotene’ vinavyobadilishwa mwilini kuwa vitamin
A; kuongeza mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa na pia kuwafanya
walaji waonekane vijana zaidi.
Faida nyingine, kwa mujibu wa Dk. Fazel, ni kwa walaji kujipunguzia uwezekano wa kupata magonjwa ya kansa.
“Tafiti zinaonyesha kuwa watu wanaokula
vyakula vyenye wingi wa virutubisho vya beta-carotene (vilivyomo kwenye
maboga) huwa na uwezekano mdogo wa kupata baadhi ya aina za kansa,
ikiwamo ya tezi dume na kansa ya mapafu,” alisema Dk. Fazel katika
sehemu ya andiko lake ambalo lilizungumzia siyo tu mbegu za maboga bali
pia boga lenyewe.
Aliongeza kuwa maboga husaidia pia kukabili
kisukari kwa kuimarisha kiwango cha sukari mwilini; kuongeza utulivu wa
mwili pia kutokana na kuwapo kwa kiwango cha virutubisho viitwavyo
‘tryptophan’ vinavyowasaidia watu wenye matatizo ya kukosa usingizi
(insomnia).
Akizungumzia faida za mbegu za maboga, Naibu
Meneja Miradi wa Kanda kutoka Sauti Project Jhpiego Tabora, Dk. Benedict
Kafumu, alisema zina kiwango kikubwa cha madini kama ya Zinc ambayo
yana faida nyingi mwilini.
Mbali na faida alizozitaja Dk. Fazel kuhusiana
na maboga, Dk. Kafumu alisema pia huimarisha uwezo wa walaji katika
kuonja na kunusa, ukuaji wa seli mbalimbali za mwili na pia kuwa na
viinilishe vyenye kuongeza nguvu ya tendo la ndoa kwa wanaume.
“Mbegu za maboga zina vitamini E ingawa siyo
kwa kiwango kikubwa lakini hiyo husaidia afya ya ngozi. Zina protini
ambayo husaidia mwili kukabili maradhi kama kisukari, tezi dume na aina
nyingine za saratani,” alisema Dk. Kafumu.
Aliongeza kuwa faida nyingine ni kuongeza uzalishaji wa maziwa ya kiwango bora zaidi kwa kina mama wanaonyonyesha.
Aidha, Dk Kafumu alisema ni vizuri kwa walaji
kutumia zaidi mbegu za maboga zilizo mbichi kwa sababu ndizo zenye
madini zaidi kulinganisha na zile zilizokaushwa na pia wawe makini ili
kuepuka kula mbegu zilizokaa kwa muda mrefu na kushambuliwa na fangasi.
“Wanaozikaanga wahakikishe kuwa haziwi kwenye
kikaangio kwa zaidi ya dakika 15. Hii itasaidia kutozipotezea ubora
wake,” alisema Dk. Kafumu.
Mshauri wa Maendeleo ya Viwanda, Linus Gedi,
aliliambia Nipashe kuwa faida za mbegu za maboga zimeanza kufahamika kwa
wengi na baadhi huzijumuisha katika vyakula maalumu vya lishe ya
watoto, wakiwamo wakazi wengi wa mkoa wa Njombe.
“Kule Njombe, wapo kina mama huzikausha na
kuzisaga pamoja na chakula cha watoto. Hii ni lishe nzuri kwa sababu ina
virutubisho vingi muhimu na vyote hupatikana kwa pamoja kwa walaji,”
alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “UTAFITI: Mbegu za maboga zinavyosaidia nguvu za kiume kuliko supu ya pweza”
Post a Comment