Thursday, April 3, 2014
DKT: SHEIN AAGIZA HATI MILIKI YA ENEO LA UJENZI WA MNARA WA MAPINDUZI KUPATIKANA HARAKA.
Do you like this story?
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali
Mohamed Shein ameagiza kufanyika mazungumzo kati ya Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii Zanzibar ZSSF na Wizara ya Ardhi,Makaazi Maji na Nishati ili
kupatikana Hati miliki katika eneo la Ujenzi wa Mnara wa Mapinduzi
katika eneo la Michezani Mjini Zanzibar.
Hayo ameyasema leo alipofanya ziara maalum kuangalia hatua ya
ujenzi wa Mnara huo na Kiwanja cha kufurahishia watoto Kariakoo
unaosimamiwa na Mfuko huo.
Amesema kupatiwa hati miliki ya eneo la Michezani ni suala la
kukaa pamoja taasisi hizo husika kwani eneo hilo linamilikiwa na Serikali na
sio la mtu binafsi.
“Nendeni mkazungumze na watu wa Ardhi mkubaliane halafu nijue
mulipofikia haya yote ni maeneo ya Serikali,”alisema Dkt. Shein.
Alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeamua kuliendeleza eneo hilo la Michezani kwa kujenga Mnara utakao kuwa na
Maduka na Mikahawa hivyo kuna haja kukaa na wafanya biashara wa
eneo hilo kufanya mazungumzo na kuwatafutia maeneo mengine ya kuendeleza
biashara zao.
“Wafanya biashara wanapenda maeneo mazuri, sidhani kama watakataa
kupatiwa sehemu nyengine ili kuendeleza biashara zao,”aliongeza Rais wa
Zanzibar.
Aidha Dkt. Shein alifurahishwa na hatua iliofikiwa katika ujenzi
wa majengo hayo na kusema kiwanja cha Kariakoo kinapaswa kuwa cha kisasa na
bora kwani kitatoa huduma nyingi za kibiashara kitakapo malizika.
Hata hivyo alisema kiwanja cha Kariakoo kimezungukwa na
majirani hivyo upo umuhimu kukaa na majirani hao kwa mazungumzo ili
kupatikana usalama wa eneo hilo.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Abdulwakil
Haji Hafidh alisema kuwa kiwanja cha Kariakoo hadi sasa kimeshagharimu shilingi
bilioni 10 na mpaka kitakapomalizika kitagharimu shilingi bilioni 13.5 za
Tanzania.
Alisema kiwanja hicho kinatarajiwa kutoa huduma kuanzia mwakani
kwani hatua kubwa ya ujenzi imekamilika na vifaa vingi vimeshawasili na
vinasubiri kufungwa.
Abdulwakili alisema kuwa kiwanja hicho kitakuwa na huduma zote
muhimu kwa binaadamu ikiwemo maduka, mikahawa na maeneo ya kupambia
maharusi na burudani nyengine.
Aliongeza kuwa ujenzi wa kiwanja hicho utakapo
kamilika wataunda bodi maalu itakayojitegemea kukiendesha.
Wakati huo huo Dkt. Ali Muhamed Shein alitembelea eneo la Skuli ya
Sekondari ya Lumumba na kukemea tabia ya kuvamia eneo hilo kwa kuchimbwa
mchanga na kuligeuza kuwa gereji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “DKT: SHEIN AAGIZA HATI MILIKI YA ENEO LA UJENZI WA MNARA WA MAPINDUZI KUPATIKANA HARAKA.”
Post a Comment