Thursday, April 3, 2014

IKULU YAMJIBU WALIOBA.




 Ofisi ya Rais (Ikulu) imesema haikuwatupia virago wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilitoa taarifa hiyo jana ikirejea taarifa zilizomnukuu aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba akisema: “Ikulu imetutupia virago.”

Jaji Warioba alikaririwa akilalamikia jinsi yeye na makamishna wa tume, walivyoondolewa ofisini na kunyang’anywa magari kwa haraka bila kusubiri siku waliyokuwa wamepanga kufanya makabidhiano.

Taarifa ya Ikulu ilisema kifungu cha 31 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinasema shughuli za tume zinakoma baada ya Mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu la Katiba.

Ilifafanua kuwa Jaji Warioba aliwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni Machi 18, 2014 na siku iliyofuata Machi 19, 2014 na kwa mujibu wa Sheria Rais alitia saini tangazo la Serikali kuvunja tume hiyo.

Ilisema tangu mwanzo wajumbe, mwenyekiti, Sekretarieti ya Tume na Watanzania wote waliijua siku ya mwisho ya Tume kukamilisha shughuli zake, hivyo kwa mtu “kujitia ameisahau siku hiyo ni kiwango cha juu sana cha unafiki.”

“Siku hiyo ya mwisho iliwekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, na Ikulu haikuwa na madaraka wala mamlaka yoyote kubadilisha tarehe hiyo.
Hivyo, madai ya Ikulu kuitupia virago Tume ya Mabadiliko ya Katiba hayana msingi wowote na ni jambo la kutunga tu,” ilisema taarifa hiyo.

Ilisema tangu Tume ilipovunjwa, haikuwa tena na kazi ya kuandaa ripoti au Rasimu kwa sababu kazi hiyo ilikuwa imekwisha.
Kuhusu muda wa kuandika ripoti ya makabidhiano, taarifa hiyo ilihoji kuwa tangu Desemba 30, mwaka jana sekretariati ilikuwa na muda wa siku 77, ilishindwa nini kuiandaa wakati maofisa wake walikuwa wanaendelea kulipwa mshahara na Serikali.
 
Kuhusu wajumbe kutakiwa kurudisha magari Ikulu, taarifa hiyo imekiri ikitoa sababu kuwa kazi ya tume ilikuwa imemalizika na kwamba magari hayo yanatakiwa kupelekwa kwenye Bunge la Katiba mjini Dodoma.

0 Responses to “IKULU YAMJIBU WALIOBA.”

Post a Comment

More to Read