Saturday, November 15, 2014

BASATA LAWATAKA WAANDAAJI WA MASHINDANO/MATUKIO YA SANAA KUZINGATIA KANUNI NA TARATIBU ZAO




Katika mazungumzo maalum na Kituo cha Mlimani TV cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza amewasisitiza waandaaji wa matamasha na mashindano ya Sanaa na urembo kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo katika kuendesha matukio yao.

Pia,amewataka waandaaji wa mashindano na matamasha katika vitongoji kuwa makini katika kusimamia taratibu kwani ndiyo wanaoandaa washiriki ambao baadaye wanakuja kushiriki kwenye ngazi ya taifa. 

Katika hili amewataka kutumia upembuzi yakinifu kabla ya kuruhusu washiriki ama wasanii kushiriki katika matukio yao ili kukwepa aibu kwa taifa.

"Kama kuna vielelezo au nyaraka zinahitajika, waandaaji lazima waziombe kwa washiriki na wazihakiki kikamlifu. Kama kuna utata wahakikishe wanahusisha mamlaka zinazohusika mapema ili kuupata ukweli" aliongeza Mngereza.

Aidha, amesisitiza kwamba BASATA litaendelea kuwabana waendeshaji/waandaaji wa matukio ya Sanaa kwani ndiyo wenye jukumu la kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa na ndiyo wanaopewa idhini ya uendeshaji na Serikali.

“Kama katika ngazi ya vitongoji,wilaya na kanda waandaaji wangeweka msisitizo, changamoto zisingekuwepo. Kuna ulegelege wa kudhibitiwa” Aliongeza. 

Amewataka waandaaji wote kusimamia kanuni  na taratibu zao  kwa haraka pasipo kusubili mashinikizo na malalamiko kutoka kwa jamii.

0 Responses to “BASATA LAWATAKA WAANDAAJI WA MASHINDANO/MATUKIO YA SANAA KUZINGATIA KANUNI NA TARATIBU ZAO”

Post a Comment

More to Read