Tuesday, November 11, 2014
TAMKO LA IKULU:TUMEFEDHEHESWA JAJI WARIOBA KUSHAMBULIWA.
Do you like this story?
Serikali inapitia upya ulinzi wa viongozi wastaafu ili kuepuka fedheha iliyotokana na vurugu alizofanyiwa Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba hivi karibuni.
Mpango huo umeelezwa
na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue mwishoni mwa wiki, akisema
Serikali imekerwa na kufedheheshwa kutokana na tukio hilo lililotokea wakati wa
mdahalo wa Katiba Inayopendekezwa katika Hoteli ya Blue Pearl, Dar es Salaam
Novemba 2, mwaka huu.
“Kimsingi tutakachokifanya ni kupitia
upya mpango wa ulinzi wa viongozi wote waliostaafu, japokuwa huwa tunafanya
hivyo mara kwa mara, lakini kwa hili la Mzee Warioba tunaliangalia kwa umakini
wake.
“Tumekerwa sana na tukio lile,
halikutufurahisha hata kidogo kama Serikali kwa kuwa limemvunjia heshima Mzee
Warioba, yule ni mzee wetu, anahitaji heshima, kwanza heshima yake na ulinzi.”
Kauli hiyo ya Sefue
imekuja wakati mdahalo huo uliovunjika baada ya Mzee Warioba kushambuliwa,
ukiwa umetangazwa kufanyika upya Jumapili Novemba 16, mwaka huu katika hoteli
hiyohiyo.
Mjumbe wa iliyokuwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole alithibitisha jana kuandaliwa
kwa mdahalo huo kuanzia saa 9.00 alasiri siku hiyo.
Tukio la kufanyiwa
vurugu Jaji Warioba lililaaniwa na wananchi, wasomi, wanasiasa na wanaharakati
mbalimbali wakisema kuwashambulia viongozi na hasa katika mjadala wa Katiba ni
kukosa uvumilivu na ni kuashiria machafuko katika siku za usoni.
Balozi Sefue
aliongeza: “Najua si jambo zuri,
iliwahi kutokea pia kwa Mzee (Ali Hassan) Mwinyi, alipigwa kibao... sasa
kingine ni mazingira yanapotokea matukio haya, wakati mwingine ni ngumu.”
Mzee Mwinyi alipigwa
kibao Machi 10, 2009 na mmoja wa waumini wa dini ya Kiislamu katika Baraza la
Maulidi wakati Rais huyo mstaafu alipokuwa akihutubia.
Kutokana na matukio hayo,
Balozi Sefue alisema: “Watanzania
tumekuwa na tabia ya kuheshimiana lakini matukio haya yanatokea na kila mmoja
hatarajii, kinachotakiwa ni sisi tuwaheshimu wazee wetu hawa.”
Mdahalo wa wiki
iliyopita ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, ulivunjika baada ya
kutokea vurugu wakati Jaji Warioba alipokuwa akihoji vitendo vya baadhi ya watu
kutumia vibaya jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Jaji Warioba alikuwa
akihitimisha hotuba yake akichambua hoja zilizomo katika Katiba Inayopendekezwa
akilinganisha na zile zilizoachwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba iliyoandaliwa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiongoza.
Vurugu hizo zilidumu kwa takriban dakika 45 ndani ya ukumbi wa mikutano wa hoteli hiyo na msaidizi wake alimtoa ukumbini dakika 30 baada ya sakata hilo kuanza, hali iliyowapa nafasi vijana hao walioonekana kujiandaa kufanya vurugu, kumsogelea Makamu huyo wa kwanza wa rais mstaafu na kumtia msukosuko.
Vurugu hizo zilidumu kwa takriban dakika 45 ndani ya ukumbi wa mikutano wa hoteli hiyo na msaidizi wake alimtoa ukumbini dakika 30 baada ya sakata hilo kuanza, hali iliyowapa nafasi vijana hao walioonekana kujiandaa kufanya vurugu, kumsogelea Makamu huyo wa kwanza wa rais mstaafu na kumtia msukosuko.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TAMKO LA IKULU:TUMEFEDHEHESWA JAJI WARIOBA KUSHAMBULIWA.”
Post a Comment