Wednesday, November 26, 2014
UMEIPATA HII KUHUSU KUWEKA PICHA YA MTOTO WAKO KWENYE MITANDAO?
Do you like this story?
Nianze kwa kukuuliza
wewe mzazi; unapoweka picha ya mtoto wako kila hatua tangu akiwa mchanga hadi
anaanza kutembea na kuanza shule, alikuomba au ulipata ruhusa yake?
Ingekuwa wewe
umepigwa picha bila idhini yako halafu ukaikuta kwenye mtandao utafurahi?
Najua unampenda mtoto
wako na ana haki zake za msingi pamoja na kuheshimiwa faragha yake popote
alipo. Haiwezekani chochote anachofanya ukiweke kwenye mtandao.
Naomba kueleza
madhara yanayoweza kutokea kwa kuweka picha za mtoto wako au wa mwenzako kwenye
mitandao hasa mitandao ya kijamii kama facebook, instagram na mingineyo.
Kwanza fahamu kuwa
kampuni karibu zote za mitandao ya kijamii zimesajiliwa Marekani, chache
zimesajiliwa Ulaya na Asia, lakini karibu zote zinatumia sheria na sera za
mataifa hayo.
Katika mataifa hayo
wanasisitiza mtoto asijiunge kwenye mitandao ya kijamii hadi atakapofikisha
miaka 13, wengine miaka 15 au 16 .
Kampuni zote za
mawasiliano zina utaratibu wa kuhifadhi kila kitu kinachotokea kwenye shughuli
zao za kila siku kwenye chombo maalumu cha kuhifadhi taarifa za mtandao
(server). Kwa hiyo ukiweka picha za mtoto zinahifadhiwa huko hata kama
utazifuta.
Hapo awali, nilisema
mtoto anahitaji faragha yake, unaporusha picha za mtoto wako kwenye hii
mitandao au mawasiliano yoyote, unaingilia faragha yake na huko mbele anaweza
kukushtaki wewe au wengine walioingilia faragha yake.
Mtoto anatakiwa
kufunzwa kuanzia mdogo kabisa kuhusu faragha yake, nini cha kusema au kutoa na
nini asiseme au asitoe. Hii ni pamoja na kwenye mitandao ya kijamii, simu na
huduma nyingine za mawasiliano .
Umeshawahi kuona
wanasiasa wanaweka picha za watoto wao au ndugu zao wa karibu kwenye mitandao
hasa ya kijamii ? unajua ni kwa nini ?
Kwa sababu kila
anachofanya yeye kinamwathiri mtoto wake au watu wake wa karibu kwa ubaya au
uzuri. Ni rahisi kuweka rehani faragha za watoto na ndugu zake.
Kama ni mtoto wa kike
anaweza kuanza kufuatiliwa na ‘mabazazi’ kwa sababu ya picha tu. Watatafuta
anapoishi, shule anayosoma na usishangae siku moja akabakwa.
Siku hizi kuna
biashara ya kutangaza ngono mitandaoni ukiweka picha ya mtoto hujui kina nani
wanaangalia na kwa matumizi gani. Wapo wanaoweza kuitumia picha hiyo kutangaza
kuwa mwenye picha anafanya biashara ya ngono, utajisikiaje kama mzazi?
Hata hivyo, picha ya
mtoto wako inaweza kutumika kutangaza biashara fulani bila wewe kujua. Haya
yameshatokea.
Kwa kuweka picha ya
mtoto wako, unatoa fursa ya kunyanyaswa na kufanyiwa vituko vingine mbalimbali
shuleni au popote atakapokwenda au kwenye kurasa zake mwenyewe za facebook.
Pia siku hizi kuna
mitandao na tovuti nyingi zinazotengenezwa kila siku, mtu anaweza kutumia picha
ya mtoto wako kutangaza tovuti yake, blogu au bidhaa zake mbalimbali bila
ruhusa yako wala ya mtoto wako.
Jijini Dar es Salaam
kuliwahi kutokea mzazi kufiwa na mtoto wake maeneo ya Kimara, aliposambaza
picha akaweka ya mfano, kumbe picha hiyo ni ya mtu mwingine, watu kwenye
mtandao wakajua ndio mtoto halisi.
Sikutishi ila
nasisitiza mzazi uheshimu faragha ya mtoto wako na taarifa zake nyingine zinazomuhusu.
Na Yona Fares,Mwananchi
Na Yona Fares,Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “UMEIPATA HII KUHUSU KUWEKA PICHA YA MTOTO WAKO KWENYE MITANDAO? ”
Post a Comment