Saturday, March 7, 2015

WATOTO WATANO WAZIKWA MAKABURI MAWILI.......SWRIKALIYAAMURU MIILI IFUKULIWE.




Wakazi wa Kijiji cha Mwakata, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, jana walilazimika kufukua makaburi mawili walimokuwa wamezika watoto watano wa familia moja waliofariki dunia juzi baada ya mvua kubwa ya mawe kunyesha kijijini hapo.

Ufukuaji wa kaburi hilo ulifanyika mchana na kuitoa miili ya watoto hao, Luku Masemba (14), Paschal Masemba (11), Mulyante Masemba (9), Sesela Masemba (7) na Masele Masemba (5).

Taarifa zilizopatikana zinasema kuwa kaburi hilo lilifukuliwa baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, kuagiza lifukuliwe ili marehemu hao wazikwe kila mmoja katika kaburi lake.

Kabla ya agizo hilo lililotolewa na Mpesya mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Rufunga, miili ya watoto watatu wote wa kike ilikuwa imezikwa katika kaburi moja.

Wakati watoto hao wa kike walikuwa wamezikwa katika kaburi moja, maiti mbili za watoto wa kiume zilikuwa zimezikwa katika kaburi moja.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, maiti hizo zilikuwa zimefungwa kwenye mifuko ya sandarusi baada ya wananchi kukosa sanda kutokana na Serikali kuchelewa kutoa utaratibu wa namna ya kuzikwa miili hiyo.

“Nimeambiwa mmewazika hawa watoto watatu kaburi moja na wengine kaburi lao moja. Hapana, hapana, huu siyo utaratibu hata kidogo.

“Nataka hawa marehemu wafukuliwe na kila mmoja azikwe kwenye kaburi lake siyo kama mlivyofanya ninyi.

“Suala la kuzikwa watu kwa pamoja labda itokee hawatambuliki na ndugu zao hawajajitokeza.

“Hawa watoto ni wa familia moja na mnawafahamu kwa majina na umri wao, iweje muwazike kaburi moja watatu na jingine wawili?

“Naagiza wafukuliwe na wazikwe upya katika mazingira ya binadamu,” alisema Mpesya.

Familia nyingine iliyopoteza watu watano kufuatia mafuriko hayo ni ya Donald Lubunda iliyo umbali wa kilomita moja kutoka mahali ilipo familia ya watoto hao watano.

Mahitaji ya msaada
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwakata, Shaban Jumanne, alisema zaidi ya tani 20 zinahitajika haraka kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko hayo na kwamba kati ya watu 42 waliofariki dunia, wengi wao ni watoto wa kuanzia umri wa miaka 14.

“Wakazi zaidi ya 4,370 katika kaya 456 zilizoathirika na janga hili hawana makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa na kuangushwa na mvua.

“Walioathirika zaidi wanafikia watu 300 na mbuzi 86, kuku 78, ng’ombe watano, bata zaidi ya 30 na paka zaidi ya 20 wamekufa katika maafa haya,” alisema kiongozi huyo wa Serikali.

Mbunge wa Jimbo la Msalala, Ezekiel Maige (CCM), alisema yeye binafsi ametoa msaada wa mifuko 200 ya unga yenye thamani ya Sh milioni tatu.

Alisema maafa hayo yalitanguliwa na mafuriko mengine yaliyotokea katika Kijiji cha Segese jimboni humo na kuharibu nyumba zaidi ya 55.

Pamoja na hayo, alimuomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waende kijijini hapo kuwasaidia waathirika hao.

0 Responses to “WATOTO WATANO WAZIKWA MAKABURI MAWILI.......SWRIKALIYAAMURU MIILI IFUKULIWE.”

Post a Comment

More to Read