Tuesday, June 23, 2015

POLISI WAKANUSHA KUMUONEA MH. GODBLESS LEMA.




KAMANDA wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas, amesema kuwa tuhuma alizotoa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema si za kweli.

Kamanda huyo alisema madai kwamba polisi wanamuonea Lema kwa kumkamata na kumweka mahabusu wakati yeye siyo mhalifu siyo za kweli na kwamba yeye (Lema) ni chanzo cha vurugu katika uandikishwaji wa daftari la wapigakura.

Akizungumza jana kwa njia ya simu jana Sabas amesema Lema anasababisha vurugu kwa kutembelea maeneo ambayo watu wamejitokeza na kujiandikisha na kuanza kupiga hotuba kitu ambacho kinyume cha sheria.

Alisema Lema kama anataka kuhamasisha watu hatukatai, aende maeneo ambayo daftari bado halijafika akahamasishe na likifika aache wananchi wajiandikishe na siyo kuwafuata kwenye mistari na kuanza kupiga hatuba, siyo sahihi.

Alisema polisi hawawezi kuonea mtu wala yeye mbunge, isipokuwa likipata taarifa kama siku ya tukio ya Juni 20 alipokamatwa kuwa analeta vurugu na wananchi hawataki kumwona katika maeneo ya uandikishaji ndipo walipokwenda kumkamata.

Alisema siku ya tukio walipata taarifa toka kwa askari walioko doria kwenye kituo cha Osunyai kuwa kuna vurugu toka kwa mbunge na kuomba ulinzi uongezwe na askari wakapelekwa zaidi na kumtia mbaroni na wenzake 24 na kuwa jumla ya watuhumiwa 25 walikamatwa na siyo yeye aliyetoa taarifa Polisi kuomba ulinzi.


Hata hivyo uchunguzi dhidi ya tuhuma zake unaendelea na upelelezi ukikamilika atachukuliwa hatua stahiki.
Awali Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, aliyekamatwa alilalamikia Polisi, kwa kumkamata na kumweka mahabusu masaa kadhaa juzi wakati akiwa kwenye kata ya Osunyai Manispaa ya Arusha, akizungukia waandikishwaji wa daftari la wapiga kura, ili kujionea hali halisi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Lema alisema ameshangazwa na kitendo hicho kwani yeye ndiyo aliyewaita polisi ili kumsaidizi ulinzi, baada ya kuvamiwa kwa kupigwa mawe na kundi la vijana wanaosadikiwa kuwa wa kundi la mgombea ubunge wa chama cha CCM.

Alisema mara baada ya kupiga simu Polisi kuomba msaada polisi walifika kwa haraka, lakini badala ya kukamata vijana hao ambao walikuwa wakizuia watu kujipanga mstari kwa madai siyo wakazi wa maeneo hayo kwa madai wakazi wa maeneo hayo Wamasai na Waarusha, wakanikamata mimi na wafuasi wangu 25 na kutuweka mahabusu.

Alisema walikaa ndani Juni 20 mwaka huu, kuanzia saa 1:30 usiku hadi saa 4:00 usiku na kuwataka wajidhamini wenyewe, kisha kuwaachia.

Lema alisema yeye ni kiongozi na sheria inamtaka ahamasishe watu kujitokeza na kujiandikisha na inapobidi kutoa elimu, lakini, hapaswi kudhalilishwa kwa kuwekwa mahabusu kwa kejeli na dharau.

“Hawa watu wanaopita kwenye kata za wenyeji na gari aina ya Land Cruiser yenye namba T.122 ATR na wakati mwingine hubadilisha kibao na kusomeka T. 122 ABR, na kuwatoa watu kwenye mistari kwa madai siyo wakazi wa maeneo hayo wakati wameuza maeneo na watu wamechanganyikana, walipaswa wakamatwe, badala yake wanakamata mbunge na watu wake kuwa wanahamasisha fujo, hiyo siyo haki,” amesema.

Alisema kazi aliyofanya kubwa ya uhamasisha watu kujiandikisha na mwamko mkubwa na hataacha kufanya hivyo, kwani ilifika mahali watu wanalala vituoni wake wa watu, akalalamika kwa kumpigia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Damian Lubuva ambaye ameongeza mashine za BVR 60 na tayari mashine 25 zimeongezwa maeneo yenye wapiga kura wengi.

Aidha alisema katika tukio la kurushiwa mawe mlinzi wake, Abdallah Mazengo alipigwa jiwe kichwani na kuzimia kwa masaa kadhaa, hata hivyo hali yake inaendelea vizuri.

Lema amemwagiza Katibu wake, Innocent Kisanyage amwandikie barua Kamanda wa Polisi mkoa huo, ili kuomba ulinzi wa Polisi kwa mbunge anapokuwa katika ziara za kutembelea kata hizo zenye uandikishwaji.

0 Responses to “ POLISI WAKANUSHA KUMUONEA MH. GODBLESS LEMA.”

Post a Comment

More to Read