Thursday, June 4, 2015
BILAL, MAGUFULI WAIBUKIA DODOMA.
Do you like this story?
WANACHAMA watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
leo wanatarajiwa kuchukua fomu, kuomba ridhaa ya uteuzi wa kuwania urais wa Tanzania,
wakati wakiwa hawajatangaza nia kama ilivyo kwa wengi wao.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na
Katibu Msaidizi wa Siasa na Ushirikiano wa Kimataifa katika Ofisi Ndogo ya CCM,
Dar es Salaam, Amos Robert wanachukua fomu leo mjini hapa.
Watatu hao ambao hawajatangaza nia ya kuwania
nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi wakipitia CCM, wataungana na mawaziri
wakuu wa zamani, Frederick Sumaye, Edward Lowassa na Balozi Ali Karume kuchukua
fomu leo.
Sumaye, Lowassa na Karume wote
wamekwishatangaza nia ya kumrithi Rais Kikwete, tofauti na Dk Bilal, Magufuli
na Robert ambao hawajatangaza popote nia yao.
Kwa mujibu wa Katibu wa Halmshauri Kuu ya
Taifa ya CCM (NEC) wa Oganaizesheni, Dk Muhammed Seif Khatib, Robert atakuwa wa
kwanza kuchukua fomu leo kuanzia saa nne asubuhi katika Makao Makuu ya CCM.
Dk Khatib alisema Katibu Msaidizi huyo
atafuatiwa na Sumaye saa 5:30 asubuhi, Dk Bilal atafuata saa saba kamili,
Balozi Karume saa 8:30 mchana, Lowassa ambaye aliahirisha jana atafuata saa
9:30 alasiri na Magufuli atafunga dimba kwa leo atakapochukua saa 10:30 jioni.
Lowassa aliahirisha kuchukua jana baada ya
kuelezwa kuwa ilitokana na kushiriki kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Ukonga,
marehemu Eugen Mwaiposa, ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati yake ya Mambo ya
Nje ya Bunge la Tanzania.
Aliagwa bungeni. Dk Bilal alikuwa mmoja wa
wanaCCM waliowania urais wa Zanzibar mwaka 2010 na alishindwa na Rais Dk Ali
Mohammed Shein katika uteuzi wa CCM.
Rais Kikwete baadaye alimpendekeza kuwa
Mgombea Mwenza na aliposhinda awamu yake hiyo ya pili kuiongoza nchini, akawa
Makamu wa Rais.
Dk Magufuli amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa
wanaCCM wanaofaa kwa urais wa Tanzania, na hajawahi kutangaza nia yake, ingawa
vyombo vya habari vimekuwa vikimtaja kuwa miongoni mwa wanaofikiria nafasi
hiyo.
Awali jana, wagombea wanne waliokwisha
kutangaza nia, walifungua pazi la uchukuaji fomu za uteuzi wa CCM ambazo
zitatolewa hadi Julai 2, mwaka huu.
Wa kwanza aliyekabidhiwa fomu na Dk Khatib
alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya
akifuatiwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira, Balozi wa
Umoja wa Afrika (AU) Marekani, Amina Salum Ali na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki,
Charles Makongoro Nyerere.
Profesa Mwandosya akifuatana na mkewe Lucy,
aliwaambia waandishi wa habari kuwa baada ya kushika nafasi ya tatu nyuma ya
Rais Kikwete na Dk Salim Ahmed Salim mwaka 2005, anaamini sasa zamu ni yake.
“Uamuzi wa kuchukua fomu ni uamuzi mzito
sana, inabidi ujiandae kisaikolojia kwa maana ya kiakili, kiafya, kimaono,
dhamira na dhima. Lakini kubwa zaidi huwezi kuwa na kiburi kama hutokani na
wananchi wenyewe au huwawakilishi, kwa hiyo ni dhima kubwa,” alisema.
Profesa Mwandosya aliongeza, “Chimwaga
nilikuwa wa tatu, huko sio kushindwa. Nikasema nimepata shaba si haba, sasa
yule wa pili hayupo, kwa hiyo, naamini ni wakati wa kupata dhahabu.
Ofisi yangu sasa iko ghorofa ya chini,
ninachoomba ni kupanda ngazi.” Kwa upande wake, Wassira naye akifuatana na
mkewe, alisema uzoefu wa muda mrefu serikalini pamoja na uchapakazi na uadilifu
wake, ni miongoni mwa sababu zinazomfanya aombe ridhaa ya uteuzi huo.
“Kwa hiyo, naomba nianze safari, siyo safari
kama ile nyingine, hii ni safari ya uhakika ya kutafuta fursa, kwa nia, kwa
uwezo, na sababu ninao uzoefu, hili sio jambo la bahati mbaya.
Nimeandaliwa na niko tayari,” alisema. Balozi
Amina akifuatana na waliowahi kuwa viongozi wenzake wa Umoja wa Wanawake wa CCM
(UWT), Anna Abdallah na Halima Mamuya, alisema atajenga uchumi imara wa
kuiwezesha Tanzania ijitegemee.
Alisema chini ya kaulimbiu yake ya ‘Matumaini
Mapya kwa Kizazi Kipya,’ atazingatia mambo makuu matatu ambayo ni kuongeza kasi
ya ukuaji wa uchumi kwa kupanga upya vipaumbele vya maendeleo kwa kutumia
vizuri rasilimali za nchi ili ziwanufaishe wananchi.
Alisema anayo nia thabiti, uwezo na uzoefu wa
kutosha kuizusha Tanzania kutoka ilipo sasa, huku akiahidi kuanzisha Mahakama
Maalumu ya kushughulikia rushwa kwani alikiri ni rushwa na ufisadi ni tatizo
kubwa sasa.
Kuhusu kama Tanzania iko tayari kwa Rais
mwanamke, alisema, “takwimu zinaonesha kuwa nusu ya Watanzania ni wanawake, na
kwa sababu hiyo, wanao uwezo wa kutoa rais.
Lakini kubwa wanawake ni waadilifu na
waaminifu, wanao uwezo wa kupambana na rushwa na ufisadi, na hata katika
matukio haya, ni nadra kuwakuta.”
Aliyefunga pazia jana alikuwa Charles
Makongoro Nyerere, ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na sasa
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Makongoro alizungumzia kwa kirefu rushwa
ilivyo tatizo sasa ndani ya CCM na kutaka zichukuliwe hatua kukabiliana na
tatizo hilo haraka iwezekanavyo.
“Rushwa ikitawala katika chama ni hatari
sana, kwani kwa kuwa kina uhusiano na serikali, basi hata huko hali itakuwa
mbaya. Rushwa inaleta heshima mbaya.
“Mwenyekiti wetu wa CCM, Rais Kikwete
amewaambia waache rushwa, lakini hawaachi. Rais wetu siyo dhaifu, ila mstaarabu
na mwenye huruma, lakini wanamuangusha sana.
Nasema turudishieni chama chetu,” alisema.
Makongoro aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa zamani wa Mkoa wa Mara, alifuatana na
wazee tisa kutoka Zanzibar, na kueleza kuwa mdhamini wake wa kwanza Zanzibar
atakuwa Rais wa Awamu ya Tano, Salmin Amour Juma maarufu kwa jina la Komandoo.
Baada ya kukabidhiwa fomu hizo, wagombea hao
walianza kusaka saini za wadhamini 450 katika mikoa ya 15 ya Tanzania Bara na
mikoa mitatu ya Tanzania Zanzibar, ikiwamo ya Unguja na Pemba.
Wakati huo huo, Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja atatangaza nia ya kugombea urais katika ukumbi wa Benki Kuu (BoT) mjini
Mwanza leo.CHANZO: HABARI
LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BILAL, MAGUFULI WAIBUKIA DODOMA.”
Post a Comment