Monday, June 22, 2015

HATARI: " WENYE UMRI 10-24 WANA HATARI ZAIDI VVU"




IMEELEZWA kuwa, vijana wenye umri kati ya miaka 10 hadi 24 wanakabiliwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), mimba za utoto na vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua jambo ambacho linadhoofisha nguvu kazi ya taifa.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Faisal Issa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa uhamasishaji juu ya afya ya uzazi na maendeleo ya vijana.
Dk. Issa amesema, vijana walio na umri katia ya miaka 10 hadi 24 wapo katika kipindi cha mabadiliko ya kisaikolojia na kimwili.

Amesema, vijana wanaotegemewa na taifa lakini wamejiingiza katika ngono zembe pamoja na kuoa au kuolewa wakiwa katika umri mdogo kitendo ambacho kinasababisha kundi hilo kuishi na VVU na vifo wakati wa kujifungua.

Dk. Issa amesema, takwimu za sensa ya 2012 zinaonesha vijana nchini ni zaidi ya silimia  31 ambapo kundi  hilo lipo katika hatari ya kukumbwa na matatizo ya afya ya uzazi, magonjwa ya kuambukizwa kwa njia ya ngono.

Amesema kuwa, kiwango cha vifo vya wanawake vinavyotokana na matatizo ya uzazi kitaifa ni 454 kati ya 100,000. Mimba katika umri mdogo kuchangia mara mbili hadi tano ya vifo, kwa Mkoa wa Mwanza jumla ya akina mama waliohudhuria kliniki ni 131,536 lakini kati ya hao 27,727 ni vijana wa chini ya umi wa miaka 20 ambao ni asilimia 21.
“Kiwango cha vifo vya wanawake vitokanavyo na uzani ni 112 kwa kila vizazi hao 100,000 kwa mwaka 2010 lakini mwaka 2014, jumla ya vifo 113 vilitokea kati ya vifo hao 100,000 ambapo kati ya hivyo vifo 40 vilikuwa kwa upande wa vijana chini ya miaka 24 ambayo ni asiliamia 35.

“Kwa upande  wa magonjwa ya kuambukizwa kwa ngono, imeonekana vijana ni moja ya kundi ambalo linaathirika sana, kwa mfano kiwango cha kitaifa cha maambukizi  kwa vijana walio na umri kati ya 15-24 ni asilimia 6.8, kwa mkoa wa Mwanza pekee  maambukizi kwa vijana ni asilimia 2.3 kwa takwimu za mwaka 2014, hii ni hatari kubwa sana,”amesema.

Dk. Issa amesema, kutokana na hali hiyo, serikali kupitia Wizara ya Afya naUstawi wa Jamii, Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto wameamua kuanzisha semina maalumu ya elimu kwa makundi hayo ili kubadili tabia na kupunguza maambukizo ya VVU na vifo vya uzazi.

Mratibu wa Afya ya Uzazi kwa Vijana kutoka Wizara ya Afya, Dk. Elizabeth Mapela amesema,  vijana ni kundi linalopaswa kupewa kipaumbele, hivyo serikali imejipanga kuokoa kundi hilo kwa kutoa elimu mikoa yote ya Tanzania Bara.


0 Responses to “HATARI: " WENYE UMRI 10-24 WANA HATARI ZAIDI VVU"”

Post a Comment

More to Read