Sunday, June 7, 2015

TFF SASA ‘YAWAONDOA’ YANGA NYOTA WA GHANA.




Ndoto za Yanga kusajili wachezaji wawili wa kigeni kutoka Ghana zinaelekea kugonga mwamba baada ya kocha Hans van der Pluijm kurejea nchini bila nyota hao.

Awali, Pluijm alielezwa kuwa angerejea nchini na wachezaji hao wawili wa kigeni kwa ajili ya kuongeza kina kwenye kikosi chake ambacho msimu ujao kitaiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na kutetea taji la ubingwa wa Ligi Kuu.

Hata hivyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndilo linalobebeshwa lawama kuwa chanzo cha kutowasajili kwa wachezaji hao, raia wa Ghana.

Imeelezwa kuwa ukimya wa TFF kutojibu maombi ya Yanga kuhusu kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka watano waliopo sasa hadi wanane ndiyo sababu kubwa ya Pluijm kurejea nchini mikono mitupu, akiwaacha nyuma wachezaji wake hao ili kuepusha gharama.

Pluijm alitarajiwa kuwasili nchini saa 6.00 usiku wa kuamkia leo akitokea Ghana anakoishi.
Kocha huyo alikwenda Ghana kwa mapumziko baada ya ligi kumalizika na timu yake kutwaa ubingwa na alitarajia leo au kesho kutoa mipango yake kuhusu timu yake tayari kwa msimu ujao.

Hata hivyo, wakati Pluijm akiwa mapumzikoni, ilidaiwa kuwa atakaporejea nchini atakuja na wachezaji wawili, kiungo na winga mahiri kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi chake, hasa kwenye michezo ya kimataifa msimu ujao.

Katibu mkuu wa klabu hiyo, Dk Jonas Tiboroha, alipoulizwa alisema mpango wa kusaka wachezaji wa kimataifa upo, lakini kikwazo ni TFF kuchelewa kutoa msimamo wao juu ya ombi la kutaka idadi ya wachezaji wa kigeni kuongezeka kutoka watano hadi wanane.

“Kweli, kuna wachezaji wa kigeni tunawafuatilia, lakini kwenye kikosi chetu mpaka sasa tumejaza nafasi za wageni, hivyo tunasubiri kwanza tamko la TFF ili tuangalie nini cha kufanya,” alisema Dk Tiboroha.

Wachezaji wa kigeni walioko Yanga ni; Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite (Rwanda), Amissi Tambwe (Burundi), Andrey Coutinho (Brazil) na Kpah Sherman (Liberia).

Mmoja wa viongozi wa Yanga amesema  kuwa Pljuim aliyetarajiwa kurejea saa 6.00 usiku wa kuamkia leo angerejea na wachezaji hao wanaochezea timu moja inayoshiriki Ligi Kuu ya Ghana, lakini mambo yamekuwa tofauti.

Naye meneja wa Yanga, Hafidh Salehe alisema Pluijm alitarajia kurejea usiku wa kuamkia leo, lakini hatorejea na wachezaji kama ilivyotajwa awali. “Kweli, kocha anarejea, lakini hatakuja na wachezaji ambao alipanga kuja nao, siwezi kusema kwa nini haji nao, ila, ngoja afike atatoa mipango yake kwa ajili ya timu,”alisema Hafidh.
CHANZO: MWANANCHI

0 Responses to “TFF SASA ‘YAWAONDOA’ YANGA NYOTA WA GHANA.”

Post a Comment

More to Read