Friday, December 11, 2015
WAFANYABIASHARA WALIOPITISHA MAKONTENA 349, KULIPA FAINI YA 28.3 KILA KONTENA
Do you like this story?
Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) imewagomea kulipa kodi bila adhabu baadhi ya wamiliki wa
makontena, ambayo yalitoroshwa kwenye bandari kavu bila kulipiwa kodi.
Badala yake,
TRA imewapelekea hati ya malipo inayowataka wafanyabiashara hao, kuhakikisha
wanalipa kodi hiyo na adhabu ndani ya siku saba, la sivyo watafikishwa
mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Hatua hiyo
inatokana na baadhi ya wamiliki wa makontena hayo, kuiomba TRA kuwasamehe
kulipa adhabu waliyopewa badala yake waruhusiwe tu kulipa kodi stahiki ya
Serikali.
Jumla ya
makontena 349 yalitoroshwa katika bandari kavu bila kulipa kodi na kuikosesha
Seri kali mapato ya Sh bilioni 80.
Wafanyabiashara
hao, pia wameomba waruhusiwe kulipa kodi wanayotakiwa kulipa kidogo kidogo kwa
madai kuwa wengine hawana uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha kutokana na
kutapeliwa na mawakala wao waliowatumia kwenda kulipa kodi hiyo.
Wakizungumza na
wanahabari, baadhi ya wafanyabiashara hao walisema agizo la Dk Magufuli
alilotoa Desemba 3, mwaka huu kuwa linawataka walipe kodi hiyo ndani ya siku
saba.
Lakini
wafanyabiashara walisema nyaraka za malipo walizopelekewa na TRA, zimewataka
kulipa kodi na faini kwa pamoja wakati hizo siku saba alizotoa Dk Magufuli
hazijamalizika.
Wafanyabiashara
hao wanadai kuwa walishalipa kodi hiyo kupitia kwa wakala wao, kama taratibu za
TRA zinavyowataka kuwatumia mawakala wa bandarini kulipa kodi, lakini kwa
bahati mbaya wakala huyo hakufikisha kodi hiyo serikalini.
Walidai kuwa
walifuatilia nyaraka za kodi kwa wakala wetu, lakini akawa anawaambia wasubiri.
“Tunaomba
hii adhabu tusamehewe, kwani sio kosa letu ila tuko tayari kulipa kodi halali
ya Serikali, lakini wakala wetu ndiye katuingiza kwenye matatizo haya na yeye
tayari ameshatoroka,” aliongeza mfanyabiashara huyo.
Katika nyaraka
za kodi ambazo TRA imewapelekea, kontena moja linatakiwa kulipiwa ushuru wa Sh
milioni 40.5 ndani ya siku saba na adhabu ya Sh milioni 28.3.
Hivyo jumla wanatakiwa kulipa Sh milioni 68.8 kama ushuru na adhabu.
Akizungumza na
mwandishi kuhusu madai hayo ya wafanyabiashara, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na
Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema adhabu walizoandikiwa
wafanyabiashara hizo, wanatakiwa kuzilipa pamoja na kodi stahiki ndani ya siku
saba.
Alisema
wamewawekea adhabu hiyo kutokana na kitendo chao cha kuiibia Serikali na kwa
taratibu za nchi, walitakiwa wawe mahabusu sasa hivi, lakini wametakiwa kulipa
ushuru wa Serikali wakati wakiwa nje; hivyo wanastahili kulipa kiasi hicho cha
fedha kama adhabu ya kukwepa kodi.
“Hawa
walitakiwa kukamatwa na kuwekwa ndani, walitoa kontena nje ya utaratibu, adhabu
hiyo ni ya kutoa makontena bila kulipa kodi,” alisema Kayombo.
“Wakishindwa
kulipa ndani ya muda huo tutawakamata tena na kuwafikisha mahakamani,” alieleza.
Kayombo
alifafanua kuwa siku saba hizo walizopewa wafanyabiashara hao ni kusamehewa
kutoshitakiwa mahakamani na sio kusamehewa kulipa adhabu wakati tayari walishakiuka
taratibu.
Alisema
wafanyabiashara hao, wachague kulipa ndani ya siku saba wasishitakiwe au waache
ili wakutane na rungu la dola la kufikishwa mahakamani.
Alisema hadi
sasa TRA imeshakusanya Sh bilioni 9.4 kati ya Sh bilioni 80 zinazotakiwa
kulipwa kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara hao waliokwepa kodi.
CREDIT:
MPEKUZI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAFANYABIASHARA WALIOPITISHA MAKONTENA 349, KULIPA FAINI YA 28.3 KILA KONTENA ”
Post a Comment