Tuesday, January 12, 2016
LEO NI MAPINDUZI YA ZANZIBAR, MGOGORO UTATULIWE.
Do you like this story?
NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha
kuiona siku ya leo.Baada ya kusema hayo nikumbushe tu kwamba leo ni siku ya
kumbukumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964.
Lakini tofauti na miaka mingine mwaka huu
siku hiyo inaadhimishwa kukiwa na mgogoro mzito wa kisiasa kati ya vyama vikuu
vya kisiasa Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF)
mara tu baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka jana.
Mgogoro huo uliibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha kutangaza kufutwa kwa
uchaguzi huo Novembar 28 mwaka jana kwa madai kuwa kuna taratibu na sheria
zilivurugwa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Hata hivyo, Mgombea Urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi akasema kwamba alikuwa ameshinda na ndiyo maana uchaguzi huo umefutwa. Kilichofuata ni mgogoro unaotishia amani visiwani humo.
Nichukue nafasi hii kumuomba Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kushughulikia mgogoro huo wa
uchaguzi Zanzibar kwa haraka ili usiweze kuleta mpasuko utakaosababisha
machafuko ya kisiasa nchini humo.
Hali ya kisiasa Zanzibar kwa sasa si nzuri hivyo ni vyema Rais Magufuli angelipa uzito wa kipekee na kulishughulikia suala hilo kwa kasi ya haraka.
Wito wangu huu unaungwa mkono na baadhi ya
wachambuzi wa masuala ya siasa ambao wameshauzungumzia mzozo wa kisiasa huo
unaoendelea visiwani Zanzibar baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar-ZEC kufuta
uchaguzi mkuu visiwani humo.
Najua kuna taarifa kadhaa juu ya juhudi za
kuupatia ufumbuzi mgogoro huo wa kisiasa Zanzibar ikiwemo mazungumzo baina ya
viongozi wa juu na wakuu wa vyombo vya usalama, wachambuzi mbalimbali wa
masuala ya kisiasa nchini walikuwa na maoni tofauti juu ya suluhisho la mzozo
huo kwa sasa ambapo Chama Cha Wananchi CUF kupitia mgombea wake visiwani humo
Maalim Seif Shariff Hamad, kikidai kuwepo mizengwe ya makusudi kuwanyima
ushindi.
Niliwahi kumsikia Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam Dk. Benson Bana, katika mahojiano maalum na chombo kimoja cha
habari akitaka kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa kama ilivyokuwa wakati wa
kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo uliomaliza mgogoro wa
kisiasa wa muda mrefu.
Kwa upande wangu naamini kwamba viongozi wa
ndani ya Tanzania wana uwezo wa kusuluhisha mgogoro huo wa kisiasa na kuumaliza
bila kuleta madhara yoyote.
Niiombe Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na vyama vya CUF na CCM kutafuta muafaka kwa njia ya mazungumzo kuhusiana na suala la kufutwa kwa uchaguzi huo kama njia ambayo itaepusha Zanzibar kutumbukia katika machafuko.
Yapo maswali mengi watu wanajiuliza, kama
vile Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha alipotangaza
kufuta uchaguzi wa Zanzibar kwa madai ya kuwepo kasoro nyingi katika zoezi
hilo, kwa nini hakusema tarehe ya kurudia uchaguzi?
Hakika niseme wazi kwamba mgogoro huu wa Zanzibar unatia doa taifa letu na wanaoushabikia bila shaka wana maslahi nao, lakini tuwaambie bila aibu kuwa waweke maslahi ya taifa mbele na waachane na ubinafsi kwani unaweza kutuletea matatizo mazito ambayo yanaweza kuzuilika.
Nimeambiwa CUF leo wanasusia sherehe za
Mapinduzi na kuna watu wanafurahia hilo, wakumbuke umoja ni nguvu na utengano
ni udhaifu, huu ni mpasuka mpya, tusiruhusu.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema
ukweli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ LEO NI MAPINDUZI YA ZANZIBAR, MGOGORO UTATULIWE.”
Post a Comment