Sunday, January 31, 2016

MAJALIWA ATAKA WATANZANIA WAFUNGUE SPORTS ACADEMY




WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wafungue shule za michezo yaani Sports Academy ambazo zitalenga kukusanya wahitimu wa shule za msingi na sekondari na kuwafundisha sayansi ya michezo.

Ametoa wito huo jana mchana (Jumamosi, Januari 30, 2016) kwenye uwanja wa Jamhuri wakati akizungumza na mamia ya viongozi na wananchi mbalimbali walioshiriki mashindano ya mbio za nusu marathon (km. 21 na km. 5) zilizofanyika mjini Dodoma. Mashindano hayo yalijulikana kama “HAPA KAZI TU HALF MARATHON”.

“Michezo ni sayansi kwa hiyo tunahitaji kuwafundisha vijana wetu sayansi ya michezo na kuwapa mbinu tofauti za kufaulu kwenye mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema wapo Watanzania wachache ambao wamethubutu kufungua shule za michezo na kuwataja Filbert Bayi (shule ya Filbert bayi) na Kanali Mstaafu Iddi Kipingu (shule ya Lord Baden). “Tumeona matunda ya sports academy hizo kwani zimeibua vijana ambao tayari wameshiriki michuano ya kimataifa,” alisema.(VICTOR)

Alisema michezo ina nafasi kubwa ya kulitangaza Taifa la Tanzania na ndiyo maana Serikali imeamua kuimarisha sekta ya michezo, utamaduni, sanaa na habari.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimpongeza kijana Joseph Stanford ambaye ameamua kutembea kwa miguu kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam kumuunga mkono Rais Dk. John Pombbe Magufuli kwa utendaji wake wa kazi.

Kijana Joseph (19) ambaye alikuwepo uwanja wa Jamhuri, alisema ametumia siku 13 tangu aanze safari hiyo ikiwa ni wastani wa km. 80 kwa siku. “Ninatembea kwa saa 12 kwa siku na ikifika jioni natafuta mahali penye mji na kupumzika,” alisema.

Joseph ambaye amehitimu kidato cha nne mwaka jana katika shule ya sekondari ya Mtoni iliyoko Mwanza-Mabatini, amesema hivi sasa anasubiri matokeo ya mitihani yake lakini ameguswa na utendaji kazi wa Rais Magufuli ndipo akaamua kuanzisha matembezi hayo ili kumuunga mkono.
Alipoulizwa anafanyaje anapopita kwenye maeneo ya misitu mikubwa au mapori ya kutisha, Joseph alisema hajakutana na misitu mikubwa ya kutisha isipokuwa kwenye milima ya Sekenke na eneo moja kabla ya kuingia mkoa wa Dodoma.

Joseph amesema anatarajia kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam kesho kutwa (Jumanne, Februari 2, 2016) kwani anasubiri kukutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Nape Nnauye hapo kesho.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JANUARI 31, 2016.

0 Responses to “MAJALIWA ATAKA WATANZANIA WAFUNGUE SPORTS ACADEMY ”

Post a Comment

More to Read