Tuesday, January 12, 2016
SIMBA WAFANYA MAAMUZI MAGUMU KWA KOCHA WAO
Do you like this story?
Uongozi wa Simba umefikia uamuzi wa kuachana
na Kerr baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara
na baadaye Kombe la Mapinduzi baada ya kutupwa nje ya mashindano hivi
karibuni kwenye mashindano yanayoendelea visiwani Zanzibar.
Pamoja na kutokuwa na matokeo mazuri lakini
inaonekana uongozi haujaridhishwa na uchezaji wa kikosi cha timu hiyo na mambo
yalikuwa mabaya zaidi katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar.
“Kweli kamati ya utendaji imefanya kikao cha
muda cha dharura na kukubaliana na hilo,” kilieleza chanzo kutoka Zanzibar.
“Taarifa tulizonazo ni kwamba kocha Kerr
ameitwa Dar es Salaam ambako ataondoka kesho (leo) Jumanne akiwa Dar es Salaam
ataelezwa kuhusiana na uamuzi huo wa uongozi kumtupia virago na nafasi yake
atapewa Kocha Majanja ambaye juzi aliingia mkataba kama kocha msaidizi”.
Chanzo kilipoulizwa kama uongozi hauwezi
kubadili uamuzi hiyo kesho, kilieleza: “Tunaamini hakuna nafasi hiyo, hata Kerr
mwenyewe ameishashitukia, atakuwa anajua kwamba mambo yatakuwa hivyo”.
Taarifa nyingine zimeeleza kwamba Kerr raia
wa Uingereza ameponzwa na ubishi na uongozi umekuwa ukimlaumu kutofanya kazi
kwa kujituma.
Wakati fulani, Rais wa Simba, Evans Aveva
aliwahi kujitokeza mazoezini kimyakimya wakati Simba ikijifua kwenye Uwanja wa
Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), hali iliyoonyesha wazi uongozi hauridhiki na
utendaji wa Mwingereza huyo aliyechukua nafasi ya Goran Kopunovic aliyeondoka
baada ya kutaka dau la Sh milioni 100 ili aongeze mkataba mpya Simba.
Kerr anaondoka na kuiacha Simba katika nafasi
ya tatu baada ya mechi 13 na imekusanya pointi 27 nyuma ya Yanga yenye 33 na
Azam FC kileleni ikiwa na 35.
Mwingereza huyo anaiacha Simba ikiwa
imeshinda mechi 8, sare 3 na kupoteza mbili, imefunga mabao 20 ikishika nafasi
ya tatu kwa ufungaji baada ya Yanga yenye 30 na Azam FC yenye 27 huku ikiwa
imeruhusu mabao 9, ikiwa safu bora ya ulinzi katika nafasi ya nne baada ya Azam
iliyoruhusu mabao 8, Mtibwa Sugar mabao 7 na Yanga yenye safu ngumu zaidi
imefungwa mabao matano tu.
CHANZO: salehjembe.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SIMBA WAFANYA MAAMUZI MAGUMU KWA KOCHA WAO”
Post a Comment