Thursday, September 15, 2016
SERIKALI YABARIKI WENYE JINSIA MBILI KUCHUNGUZWA
Do you like this story?
Mamlaka
ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali itakuwa na uwezo na mamlaka ya kuchunguza
watu waliozaliwa na jinsi mbili na kubaini jinsi tawala yenye nguvu zaidi.
Muswada
wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016,
uliopitishwa juzi usiku saa nne bungeni unampa Mkemia Mkuu mamlaka ya
kuchunguza na kubaini jinsi ya mtu na kutatua utata kwa mtu atakayekuwa
amezaliwa na jinsi mbili.
“Waheshimiwa
wabunge naona wengi wenu mnadhani mkemia mkuu kazi yake ni kuchunguza vinasaba
kubaini uhalali wa mzazi na mtoto, maana naona wabunge wengi wamelishabikia
hilo, lakini katika teknolojia ya vinasaba yanahusu pia utambuzi wa jinsi, watu
unakuta wanawake au wanaume wanazaliwa jinsi ya kike na kiume, kwa hiyo
tunaangalia jinsi tawala ni ipi ina nguvu,” alisema Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Ummy
alikuwa akijibu michango ya wabunge waliochangia wakati wa kujadili Muswada wa
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu 2016 kabla ya kuupitisha juzi usiku,
waliotaka mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu kutoa elimu kwa wananchi juu ya
shughuli zake.
Alisema
kwa sheria hiyo, sasa mkemia mkuu kupitia maabara yake anaweza kusema jinsi ya
kike au ya kiume ndio yenye nguvu, lakini pia kuna suala la kuhakikisha
utambuzi wa mwanadamu hasa wakati yanapotokea majanga pamoja na watu
wanaosafiri kwa makundi.
Alikubaliana
na wabunge kuwa iko haja ya kuwaelimisha wananchi juu ya kazi za maabara ya
mkemia mkuu ambao wengi wao wanadhani inafanya kazi hiyo tu ya kubaini vinasaba
vya mzazi na mtoto, lakini sasa wafahamu hata waliozaliwa na jinsi mbili
wanaweza kutegua utata huo kwa kubaini jinsi tawala au jinsi yenye nguvu zaidi
kama ni ya kiume au ya kike.
Alisema
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imekuwepo kihistoria tangu mwaka 1890 na
imekuwa chombo cha kiserikali cha uchunguzi cha kikemia wa kimaabara kwa bidhaa
mbalimbali na kuongeza kuwa imekuwa ikifanya uchunguzi wa kikemia wa vyakula,
dawa na vipodozi hasa pale inapotokea utata au kuhusisha masuala ya kesi za
jinai.
Akifafanua
zaidi, alisema kwa upande wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wao wanafanya
udhibiti wa ubora wa chakula, dawa na vipodozi na maabara hii inafanya
uchunguzi wa kikemia.
“Maabara
ya Mkemia Mkuu kazi yake ni kufanya uchunguzi wa kikemia, vinasaba, kesi za
jinai na sayansi jinai. Chombo hiki hakipimi kudhibiti ila kufanya uchunguzi
kwa ajili ya vitu vyenye maslahi ya taifa au masuala yenye utatanishi na
ushindanishi,” alisema waziri
huyo.
Akitoa
mfano wa mahindi, alisema kulikuwa na tatizo la sumu kuvu, kwa hiyo mkemia mkuu
anafanya uchunguzi wa kimaabara na kusema wamekuta mahindi yana sumu au la, au
anaweza mfanyabiashara kuleta maziwa ya mtoto TFDA ikapata mashaka, mkemia mkuu
atayafanya uchunguzi wa maabara atasema kama kuna sumu ama kuna kemikali isiyo
salama kwa matumizi wa binadamu.
“Baada
ya uchunguzi wa kimaabara mwenye jukumu la kusema mahindi haya yasiuzwe au
maziwa haya yasiuzwe ni TFDA na sio maabara ya mkemia mkuu. Vile mfanyabiashara
anaweza kuleta bidhaa, TFDA ikaitilia mashaka, kwa hiyo huyu mwenye bidhaa
anaweza kukata rufaa kwa mkemia mkuu ili apimiwe bidhaa yake kuithibitishia
TFDA kuwa bidhaa yake ni salama,”
alisema.
Waziri
Ummy alikuwa akijibu hoja za wabunge, ambao walikuwa wana hofu kuwa Maabara ya
Mkemia Mkuu inaweza kuingilia kazi za taasisi kama TFDA na Shirika la Viwango
Tanzania (TBS).
Alizungumzia
pia kuhusu kuipa mamlaka ya mwisho maabara hiyo, akisema katika nchi zote
duniani zenye maabara hizo, lazima serikali iwe na msemaji wa mwisho wa
uchunguzi wa masuala ya kimaabara na kikemia, vinasaba, sayansi jinai na kesi za
jinai, lakini pia haifuti sheria wala maabara zingine za uchunguzi
zilizoanzishwa kwa mujibu wa sheria mbalimbali.
Kuhusu
kutenga bajeti ya kutosha, Ummy alisema serikali imepokea maoni ya wabunge na
kuwa baada ya kupitisha muswada huo maabara hiyo imepewa hadhi ya mamlaka na
sasa imepewa hadhi na hivyo fungu lake lazima liwe zuri kwa ajili kuendesha
shughuli za maabara lakini pia kuajiri watumishi 400 kwani waliopo sasa 192
hawatoshi.
Waziri
Ummy alisema wamepokea ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, kufanya uchunguzi
wa matumizi ya shisha na kuongeza kuwa tayari mkemia mkuu alifanya uchunguzi na
kubaini watumiaji wa shisha wanachanganya bangi, heroine na kokeni na ndio
maana serikali ilipiga marufuku kuitumia.
Hata
hivyo, alisema sasa itajikita zaidi kuchunguza ili kubaini viambata kiasi gani
vilivyopo katika shisha na kwa nini serikali iendelee kupiga marufuku matumizi
ya shisha nchini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)


0 Responses to “ SERIKALI YABARIKI WENYE JINSIA MBILI KUCHUNGUZWA”
Post a Comment