Monday, November 28, 2016

WANUSURIKA KUFA KWA KUSHINDANA KULA CHAPATI 30 NA VIKOMBE 10 VYA CHAI




Vijana wawili wakazi wa kijiji cha Mgungira wilaya ya Ikungi mkoani hapa,wamenusurika kifo baada ya kuanza kutapika na kuishiwa nguvu katika shindano la kula chapati 30 pamoja na kunywa vikombe 10 vya chai ya rangi.

Shindano hilo la aina yake hufanyika kijijini hapo ambapo liliandaliwa,vkuratibiwa na kudhaminiwa na Guhumela Lubadila na vigezo vya kuwa mshindi ilitakiwa mshiriki ale chapati zote 30 na anywe vikombe vyote 10 vya chai ya rangi. Vitu vyote hivyo, gharama yake ni shilingi 9,200.

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Kata ya Mgungira, Hussein Juma Ng’eni, alisema washiriki walikubaliana mshindi asipewe zawadi yoyote, zawadi yake ni chapati 30 na vikombe 10 vya chai atakavyokuwa amekula na kunywa.

Aidha, alisema kuwa endapo vijana hao wakashindwa kufikia lengo la kula chapati 30 na kunywa vikombe vya chai 10, watapaswa wamlipe mmiliki wa mgahawa aliyetambulika kwa jina la mama Benja Mgungira.

Afisa mtendaji kata huyo, alisema endapo mshindi angepatikana, mdhamini wa shindano hilo, Guhumela, angemlipa mmiliki wa wa mgahawa, shilingi 9,200.

Ng’eni alisema vijana hao kama ingekuwa ni shindano la mpira wa miguu, wangekuwa wametoka suluhu ya kufungana magoli sawa kwani wao kila mmoja alikula chapati 19 na vikombe vinne vya chai ya rangi.

“Baada ya kufikia hatua hiyo, kila mmoja alianza kutapika mfululizo huku wakitokwa na jasho jingi na kisha kuishiwa nguvu. Kitendo hicho kilisababisha wakimbizwe katika zahanati ya kijiji, kupatiwa matibabu .Hali zao kwa ujumla,zinaendelea vizuri,” alisema.

Alisema kuwa baada ya kushindwa katika shindano hilo, vijana hao watalazimika kulipa shilingi 9,200 kwa mujibu wa makubaliano ya shindalo hilo.

Na Nathaniel Limu, Ikungi

0 Responses to “WANUSURIKA KUFA KWA KUSHINDANA KULA CHAPATI 30 NA VIKOMBE 10 VYA CHAI”

Post a Comment

More to Read