Monday, November 28, 2016

MJANE ALIEMLALAMIKIA RC MAKONDA KUWA KADHULUMIWA AFARIKI DUNIA GHAFLA




Mjane Halima Nyanza ambaye ni mkazi wa Chamazi, amefariki ikiwa ni saa chache kabla ya kupata ufumbuzi wa mgogoro wa ardhi.

Katika ziara iliyofanywa wiki hii wilayani Temeke, Makonda alitoa siku saba kwa Manispaa ya Wilaya ya Temeke kuutafutia ufumbuzi wa mgogoro wa ekari 10 ambazo Nyanza alilalamika kuwa amedhulumiwa.

Baada ya Makonda kutoa muda huo, uongozi wa wilaya hiyo ulipanga kukutana Alhamisi kujadili suala hilo, lakini wakati wakiwa tayari wamekusanyika wakimsubiri mlalamikaji, Diwani wa Chamazi, Hemed Karata amepokea taarifa kuwa mjane huyo amefariki dunia ghafla.

Akithibitisha taarifa hizo, Karata ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo, amesema amepokea taarifa ya kifo hicho na mazishi yalifanyika Ijumaa.

Kuhusu haki ya mjane, Karata amesema atashirikiana na uongozi wa wilaya kuhakikisha inapatikana haraka iwezekanavyo ikiwamo familia hiyo kurejeshwa eneo hilo
“Hakuna utata kwa halmashauri kutokana na ukubwa wa eneo kila mtoto alitakiwa kupewa kiwanja kimoja baada ya kupima, tumeona eneo hilo litatoa viwanja vinne na hii imetokana na ujenzi holela uliopo, lakini sehemu inayosalia tutawatafutia eneo jingine,” amesema Karata.

Mtoto wa Nyanza, Mosi Ngulangwa amethibitisha mama yake alikufa Novemba 24 saa nne siku ambayo alitakiwa kuhudhuria kikao cha kamati ili kupata ufumbuzi wa mgogoro huo.
Source: Mwananchi



0 Responses to “ MJANE ALIEMLALAMIKIA RC MAKONDA KUWA KADHULUMIWA AFARIKI DUNIA GHAFLA”

Post a Comment

More to Read