Saturday, December 31, 2016
BASI LA NATIONAL EXPRESS LAPATA AJALI SINGIDA
Do you like this story?
Watu wawili wamefariki
dunia na wengine 26 kujeruhiwa kwenye ajali iliyohusisha basi la kampuni ya
National Express T.662 DEF, baada ya kuacha barabara na kupinduka zaidi ya mara
tatu katika eneo la kijiji cha Tumuli, wilaya ya Mkalama mkoani Singida.
Waliofariki ni dereva wa basi hilo Athumani Idd (47) mkazi wa Mabibo jijini Dares Salaam na mwalimu wa shule ya msingi Malunga aliyefahamika kwa jina moja la Janet (anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 29).
Habari zilizopatikana jana
eneo la tukio, zimedai kuwa katika siku za hivi karibuni mwalimu Janet
alimpeleka mama yake jijini Dar es salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Imedaiwa kuwa baada ya
kufika Dar es Salaam, aligundua kuwa amesahau kuchukua kadi ya bima ya afya, na
hivyo akalazimika kurudi Iramba.
Jana asubuhi Janet alichelewa basi la
National Express katika kituo cha Kyengenge na kuamua kukodi bodaboda
kulifukuzia basi hilo na kufanikiwa kulikuta kituo cha Malunga. Baada kupanda
basi hilo, dakika chake baadae, basi hilo lilipata ajali na kulaliwa na basi
kichwani.
Watu hao wamefariki dunia papo hapo na
miili yao ipo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa mjini
Singida. Basi hilo lilikuwa linatokea New Kiomboi, likielekea jijini Dar.
Akizungumza kwenye eneo la tukio,
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida , ACP Debora Daudi Magiligimba,
alisema ajali hiyo imetokea Desemba, 30 saa 12.45 asubuhi katika eneo la kijiji
cha Tumuli.
Alisema ajali hiyo pia imesababisha
majeruhi 26 ambao wamelazwa katika hosipitali ya mkoa kwa ajili ya kupatiwa
matibabu.
Kamanda Magiligimba alisema uchunguzi
wa awali unaonyesha kuwa ajali hiyo kwa kiwango kikubwa imesababishwa na mwendo
kasi na uzembe.
“Eneo hili ilipotokea ajali hii kuna
mteremko na kona kali. Kutokana na mwendo kasi, dereva alishindwa kulimudu na
hivyo kuacha barabara na kuingia kwenye korogo la mto, na kuruka juu kisha
kupinduka mara tatu,” alisema.
Kwa upande wake mganga mkuu mkoa wa
Singida, Dk. John Mwombeki, alikiri kupokea miili ya watu wawili waliofariki
dunia kwenye ajali ya basi la National Express, pamoja na majeruhi 26.
“Kati ya majeruhi hawa,
mmoja dada Joyce tumempa rufaa kwenda hospitali ya taifa Muhimbili kutokana na
sehemu yake ya mwili ya chini kutokufanya kazi. Majeruhi 10 wao tunaendelea
kuwafanyia uchunguzi”alisema
Dk. Mwombeki.
Mmoja wa majeruhi hao mfanyakazi wa
shirika la TBC jijini Dar es Salaam, Victor Elia, alisema pamoja na kupoteza
kila kitu, anamshukuru Mungu kwa kupona kufa kwenye ajali hiyo mbaya.
“Kilichonisaidia ni kufunga
mkanda … abiria wenzangu wote ambao hawakufunga mikanda ndio walioumia zaidi
wakiwemo waliopoteza maisha. Ajali hii kwa vyovyote imechangiwa na mwendo
kasi,” alisema
Victor ambaye ni mtayarishaji na mtangazaji wa TBC.
Kondakta wa basi hiyo, Nicolaus
Apolinari (23) mkazi wa jijini Dar es Salaam, alisema ajali hiyo imechangiwa na
utelezi uliosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BASI LA NATIONAL EXPRESS LAPATA AJALI SINGIDA”
Post a Comment