Wednesday, December 21, 2016
RAIS MAGUFULI AKATAA SHULE KUITWA JINA LAKE
Do you like this story?
Rais John Magufuli amekataa shule ya
msingi iliyojengwa hivi karibuni eneo la Bunju, Wilaya ya Kinondoni kuitwa kwa
jina lake badala yake ameagiza iitwe kwa jina la Mkuu wa wilaya hiyo, Ally
Hapi.
Taarifa ya badiliko la jina haikutolewa
na Idara ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu kama ilivyozoeleka bali na mkuu
wa wilaya hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa mbalimbali vya usafi kwa
uongozi wa shule hiyo.
“Shule hii imejengwa kwa
fedha zilizopatikana baada ya Serikali Kuu kubana matumizi. Tukaamua iitwe John
Magufuli lakini yeye akatoa agizo shule ipewe jina la mkuu wa wilaya sina budi
kukubaliana na hilo,”alisema
Hapi.
Shule hiyo mpya iliyopo Bunju jijini
imejengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi
Bunju A ambayo ilikuwa na wanafunzi 3,224.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo mpya, Ali
Mwakapalila alisema ingawa inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 9
mwakani inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Hakuna umeme wala maji,
hii inaweza kuleta madhara kwa wanafunzi hasa linapokuja suala la matumizi ya
vyoo,” alisema.
Baada ya hafla hiyo, Hapi alikwenda
kwenye kiwanda cha saruji cha Twiga Cement ambako alipokea msaada wa mifuko 600
ya saruji kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa madarasa na majengo mengine.
Akipokea msaada huo, Hapi alisema
msaada kutoka Twiga Cement unaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano
inayoipa sekta ya elimu kipaumbele ili kuhakikisha inatolewa katika mazingira
bora.
“Msaada huu umekuja muda
muafaka. Tumeshajenga shule ila tunataka kuongeza madarasa, maabara, ofisi ya
elimu na kuzungushia uzio ili watoto wawe katika mazingira salama. Lengo ni
kuifanya shule hii iwe ya kisasa na itakuwa mfano kwa shule zote za Wilaya ya
Kinondoni,”alieleza.
Pia, Hapi alisema wilaya hiyo ipo
kwenye mipango ya kujenga maktaba ya kisasa kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya
saruji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twiga Cement,
Alfonso Velez alisema kuchangia katika shughuli za kijamii ni moja ya mambo
ambayo wamekuwa wakiyapa kipaumbele zaidi.
“Kushiriki shughuli za
maendeleo katika jamii ni jambo ambalo tunalipenda zaidi. Yalipo maendeleo
Twiga Cement ipo pia,” alisema
Velez.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ RAIS MAGUFULI AKATAA SHULE KUITWA JINA LAKE”
Post a Comment