Tuesday, February 7, 2017

HJFMRI – WRP TANZANIA YATOA MSAADA WA VIFAA KWA MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI VYA SHILINI MILIONI 226.


Mkurugenzi Mkuu wa HJFMRI – WRP Mbeya, Dk. David Elkins akisoma hotuba juu ya mkakati wa shirika la WRP kusaidia vifaa katika sekta ya afya kwa mikoa ya Nyanda za juu kusini ambayo wanatekeleza miradi



Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya anayeshughulikia Serikali za Mitaa, Costantin Mushi akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa vifaa vya mnyororo baridi vilivyotolewa na HJFMRI – WRP Mbeya kwa Mikoa mitano ya Kanda ya Nyanda za juu kusini.


Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya anayeshughulikia Serikali za Mitaa, Costantin Mushi akikata utepe kuzindua vifaa vya mnyororo baridi vilivyotolewa na HJFMRI – WRP Mbeya kwa Mikoa mitano ya Kanda ya Nyanda za juu kusini. 

Mkurugenzi wa shughuli za Maabara kutoka WRP, Dk. Julius Muhanuzi akitoa maelezo juu ya namna ya kutumia vifaa kwa mgeni rasmi ambaye ni Katibu Tawala msaidizi Mkoa wa Mbeya – Serikali za Mitaa

Baadhi ya Vifaa yakiwemo Majokofu ambayo yamekabidhiwa kwa Mikoa ya Nyanda za juu kusini na WRP




PEPFAR kupitia Shirika la  HJFMRI – WRP Tanzania limetoa msaada wa vifaa vya mnyororo baridi kwa Mikoa mitano ya Nyanda za juu kusini wenye thamani ya shilingi Milioni 226,195,970.

Akizungumza katika hafla ya kukibidhi msaada huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa niaba ya Mikoa mingine minne,Mkurugenzi Mtendaji wa HJFMRI, Dk. David Elkins alisema  vifaa vya mnyororo baridi vitasaidia utunzaji wa sampuli za damu na kuzifikisha maabara zikiwa bado na ubora unaotakiwa na baadae kupata majibu sahihi.

Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na mashine za kutenganishia damu na maji 40,majokofu madogo ya kubebea na kusafirishia sampuli za damu 40 na majokofu ya kuhifadhia sampuli  93 vyote vikiwa na thamani ya dola za kimarekani 121,215.

Alisema Mikoa itakayonufaika ni pamoja na Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Katavi na Songwe ambapo Mkoa wa Mbeya utapata majokofu 20, Ruvuma 20 huku Rukwa na Katavi zikipewa majokofu 18.

Awali akimkaribisha Mkurugenzi mtendaji, Mkurugenzi wa Ufundi wa Walter Reed Programm (WRP), Mbeya, Dk. Joseph Chintowa alisema utekelezaji wa msaada huo umetokana na maagizo ya shirika la afya duniani ambalo liliagiza kutumika kwa vifaa vya kujua idadi ya virusi vya Ukimwi kwa mgonjwa badala ya CD4.

Alisema vifaa hivyo vitahifadhiwa katika vituo vya afya ambavyo vitateuliwa kama vituo vya kukusanyia damu ambapo vifaa hivyo vinauwezo wa kutenganisha damu na maji na kuhesabu idadi ya virusi na kwamba mgonjwa anapaswa kupimwa mara mbili kwa mwaka.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, Katibu tawala msaidizi anayeshughulikia Serikali za mitaa, Costantin Mushi mbali na kulipongeza shirika hilo pia aliwaagiza waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya kuendelea kuhamasisha jamii katika kupunguza maambukizo ya VVU kwa kujitokeza kupima afya zao.

Aliongeza kuwa hata Waliokatika kutumia dawa za kufubaza VVU wanapaswa kukumbushwa kuhudhuria kliniki sambamba na watoa huduma kuomba kuwapima wingi wa virusi vya Ukimwi ili kuweza kuwa na jamii isiyokuwa na maambukizi.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina akishukuru kwa niaba ya Waganga wengine alisema ni vema Hlmashauri zitakazopewa vifaa hivyo kutenga bajeti kwa ajili ya kuviendesha vifaa ili viweze kukaa muda mrefu vikiwa salama.

Aliongeza kuwa ni vema mashirika mengine yakaiga mfano kwa HJFMRI kwa kujitikeza kutoa msaada kwani idara yta afya bado inamahitaji mengi ambayo hayajafikiwa kutokana na Serikali kuwa na vipaumbele vingi.

0 Responses to “ HJFMRI – WRP TANZANIA YATOA MSAADA WA VIFAA KWA MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI VYA SHILINI MILIONI 226.”

Post a Comment

More to Read