Friday, March 14, 2014

BILIONEA MMAREKANI AKOLEZA VITA DHIDI YA UJANGILI.




 Familia ya bilionea namba mbili nchini Marekani, Warren Buffett imeunga mkono juhudi za kupambana na ujangili nchini kwa kuchangia helikopta moja.

Familia ya Warren Buffett imeamua kutoa msaada huo kupitia Mfuko wa Howard Buffett Foundation, baada ya kuridhishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali. 

Helikopta hiyo itatumika kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya ujangili katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba nchini.
Msaada huo ulikabidhiwa juzi kwa Rais Jakaya Kikwete na mtoto wa bilionea huyo, Howard Buffett, ambaye yuko nchini kwa mapumziko ya kitalii.

Akikabidhi mfano wa helkopta kwa Rais Kikwete, Buffett alisema amevutiwa na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na ujangili hususan wa tembo na faru.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema wamepokea kwa furaha ufadhili huo, ambapo utahusisha mafunzo kwa marubani wawili nchini Marekani ama Afrika Kusini kutokana na matakwa ya wizara.

“Wametuambia pesa ipo tayari ila ni jukumu letu sisi kama Serikali kuchagua aina ya helikopta tunayoitaka. Itakuwa na uwezo wa kubeba watu sita na kwa sasa tunaangalia kama tuchukue Bell ama Ecopter, wataalamu wanashughulikia,” amesema.

0 Responses to “BILIONEA MMAREKANI AKOLEZA VITA DHIDI YA UJANGILI.”

Post a Comment

More to Read