Thursday, March 20, 2014
KIKWETE NA UJUMBE MZITO.
Do you like this story?
Rais Jakaya Kikwete kesho ataambatana na
ujumbe mzito wa marais wastaafu wa pande zote za Muungano, wake wa waasisi wa
taifa na mawaziri wakuu wastaafu atakapokwenda kuzindua Bunge Maalumu la
Katiba.
Hatua ya Rais kuambatana na ujumbe huo
imepongezwa na viongozi wa vyama vikuu vya upinzani nchini, Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba na mwenzake wa Chadema, Freeman Mbowe.
Mbali na viongozi hao, Rais Kikwete pia
ataambatana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais, Dk
Mohamed Gharib Bilal na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif
Hamad.
Wanaotarajiwa kuwamo katika msafara huo ni
Rais wa pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa tatu, Benjamin Mkapa na
marais wastaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour na Amani Abeid Karume, Mama Maria
Nyerere na Mama Fatma Karume.
Miongoni mwa mawaziri wakuu wastaafu
wanaotarajiwa kuwamo ni pamoja na Jaji Joseph Warioba, ambaye juzi aliwasilisha
bungeni hapo Rasimu ya Katiba kwa kutoa hotuba iliyoliteka Bunge kwa jinsi
alivyofafanua mambo mengi yenye utata kuhusu muundo wa Muungano.
Mawaziri wakuu wengine ni Cleopa Msuya, John
Malecela, Dk Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye pamoja na Edward Lowassa na
Mizengo Pinda ambao ni wajumbe wa bunge hilo.
Wengine walioalikwa ni mabalozi wa nchi
mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, viongozi wa dini, vyama vya
wafanyakazi, vyama vya siasa, wafugaji, wakulima, wavuvi na wawakilishi wa
sekta binafsi.
Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya
Khamis Hamad aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Rais Kikwete atahutubia
Bunge hilo kwa mujibu wa Kanuni ya 75 (1).
Rais Kikwete atapokewa katika Viwanja vya
Bunge na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na baadaye kukagua
gwaride maalumu kabla ya kuhutubia Bunge kuanzia saa 10:00 jioni.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana, baada
ya Rais kuhutubia saa 11:35 jioni, aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa bunge hilo,
Pandu Ameir Kificho atatoa neno la shukurani kabla ya Rais kupiga picha za
kumbukumbu na wajumbe wa Bunge hilo.
Suala la hotuba ya Rais Kikwete limekuwa
sehemu ya mjadala katika Bunge hilo kutokana na baadhi ya wajumbe kuhoji sababu
za Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu kabla ya Rais kuzindua Bunge kwa mujibu wa
kanuni.
Mjadala huo uliwafanya baadhi ya wajumbe
kumzuia Jaji Warioba Jumatatu iliyopita kuwasilisha rasimu hiyo kama ilivyokuwa
imepangwa hadi kilipofanyika kikao cha maridhiano siku hiyohiyo usiku na
kufikia mwafaka kwamba Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
awasilishe Rasimu juzi na Rais ahutubie kesho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “KIKWETE NA UJUMBE MZITO.”
Post a Comment