Thursday, March 13, 2014
NDEGE WA AJABU WAIKUMBA BUKOBA, KINYESI CHAO CHAUA KUKU 516, NA MBUZI 12...!!!!!
Do you like this story?
Ndege wa ajabu wakiwa juu ya miti katika Kisiwa cha Musira kilichopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera. Ndege hao wamezua hofu kwa wakazi kutokana na kinyesii chao kudhuru mifugo na ndege. |
NDEGE wa ajabu wanaosadikiwa
kutoa kinyesi chenye sumu kali, wamevamia Kisiwa cha Musira kilichopo Manispaa
ya Bukoba na kusababisha vifo vya mifugo na ndege wafugwao, huku ukali wa sumu
hiyo ukisababisha kutoboka mabati ya nyumba zilizopo kisiwani humo.
Ndege hao wanaoaminika kuvamia kisiwa hicho
mwezi mmoja uliopita tayari wameshasababisha vifo vya kuku 516 na mbuzi 12
wanaodaiwa kugusa au kula kinyesi chao.
Hata
hivyo, bado haijafahamika ndege hao wanatokea nchi gani.
Akithibitisha habari hizo, Mkuu wa Mkoa wa
Kagera, Kanali Mstaafu, Fabian Massawe alisema Serikali ilipata taarifa hizo
kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na baadaye kuundwa timu ya
kutafuta taarifa za awali za tatizo hilo.
Massawe amesema ndege hao,
pamoja na kusababisha vifo vya mifugo na ndege wafugwao pia baadhi ya miti
katika kisiwa hicho imekauka na mabati kutoboka inapotokea kinyesi chao
kitaangukia kwenye paa za nyumba zao.
Pia Massawe amesema kuwa, taarifa ya kuwapo
kwa ndege hao katika Kisiwa cha Musira, ilifikishwa kwa Naibu Waziri wa Afya,
Dk. Kebwe Stephene Kebwe aliyekuwa mkoani humo wiki iliyopita na kuwa suala la
kuwapo kwa ndege hao siyo la ghafla kwa kuwa walikuwapo hapo awali.
Dk. Kebwe alisema wizara imetuma wataalamu
kuchunguza tatizo hilo na kuwa wizara hiyo itaangalia ukubwa wa tatizo hilo
linavyoweza kuwaathiri wananchi.
Hata hivyo, alisema suala hilo pia linahitaji
ufuatiliaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Dk. Munda Elias alikwishawasili
kwa ajili ya uchunguzi na kuthibitisha kuwa tayari kinyesi cha ndege hao
kimepelekwa maabara kwa ajili ya uchunguzi na Mkoa unasubiri matokeo ya utafiti
huo.
Naye Ofisa Tarafa wa Rwamishenye, Abdon Kahwa
akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Ziporah Pangani alisema tayari
Serikali imechukua hatua za kupiga marufuku kupeleka au kusafirisha mifugo
kutoka kisiwani humo kwenda maeneo mengine kwa hofu ya kusambaa kwa sumu
hiyo.
Pia amesema ndege hao wameleta hofu kwa wakazi
wa kisiwa hicho, kwani kinyesi chao kinapodondoka kwenye bati hupata kutu na
kutoboka, huku kukiwa na hofu nyingine kwamba huenda mifugo nayo imeathiriwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “NDEGE WA AJABU WAIKUMBA BUKOBA, KINYESI CHAO CHAUA KUKU 516, NA MBUZI 12...!!!!!”
Post a Comment