Monday, March 24, 2014
NKAMIA: NITAYAFUTA, KUYAFUNGIA MAGAZETI.
Do you like this story?
Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, Juma Nkamia, |
VITISHO vya watendaji wa serikali kwa vyombo
vya habari vimezidi kushika kasi, safari hii Naibu Waziri wa Habari, Michezo na
Utamaduni, Juma Nkamia, akitishia kuvifungia au kuvifuta.
Nkamia amebainisha kuwa magazeti
yanayowachafua watu, serikali na kuhatarisha usalama wa nchi yatakumbana na
kifungo.
Itakumbukwa mwaka jana serikali ililifungia
gazeti la Mtanzania kwa miezi mitatu na Mwananchi kwa wiki mbili, kwa madai ya
kuandika habari za kichochezi.
Nkamia, alitoa vitisho hivyo jana
jijini hapa kwenye tamasha la vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Voice
of Youth (VOYC) lililokuwa likijadili masuala mbalimbali yahusuyo vijana.
Miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakijadiliwa ni
ujira, uzalendo, ujasiriamali na ajira,
Nkamia amesema hatakubali siku moja asutwe kwa kutotimiza wajibu wake katika wizara anayoisimamia, kwa kuwaachia waandishi wasiofuata maadili ya taaluma yao.
“Mimi sitaki kufanya kazi na waaandishi wa
habari makanjanja, ambao si makini na wanaofanya kazi kwa masilahi ya kundi
fulani la watu.
“Tutakifuta, kukifungia chombo chochote cha
habari pamoja na waandishi wake wanaokwenda kinyume cha maadili ya uandishi wa
habari, sitaruhusu wanaoendekeza kuwachafua wengine, umbea,” alisema.
Amesema amefanya kazi hiyo kwa kuzingatia
maadili ya taaluma hiyo kabla ya kuingia kwenye siasa ambako sasa anasimamia
wizara inayoshughulika na waandishi wa habari.
Nkamia pia alitumia fursa hiyo kuwasihi
vijana waache kushiriki kwenye maandamano yanayoitishwa na vyama vya siasa
alivyoviita havina malengo mema kwa taifa.
Alibainisha kuwa vijana hawawezi kupatiwa
fedha kama hawafanyi kazi yoyote, kwani hata mataifa yaliyoendelea ambayo ni
Marekani na Uingereza hawafanyi hivyo.
Hata hivyo katika mkutano huo, viongozi wa
halmashauri na mkoa walikacha kuhudhuria na hawakutuma wawakilishi katika
tamasha hilo licha ya kualikwa.
Kukacha kwao huko kulisababisha gumzo kubwa
na Afisa Tarafa ya Nyamagana, Maximilian Kailanga, alibeba jukumu la
kumkaribisha Nkamia.
Chanzo Tanzania Daima.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “NKAMIA: NITAYAFUTA, KUYAFUNGIA MAGAZETI.”
Post a Comment