Tuesday, March 4, 2014

PANGUA PANGUA MALIASILI YAIBUA MAPYA.


Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu


Wiki moja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kupangua wakurugenzi wizarani hupo, baadhi ya askari wa wanyamapori wameibuka na kupinga uamuzi huo, huku wakitishia kufanya mgomo

Askari hao zaidi ya 10 walioomba kutotajwa majina gazetini kwa usalama wa ajira zao, wamepinga kuondolewa kwa Prof Alexander Songorwa kwenye nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori na badala yake kuteuliwa kwa Paul Sarakikya kukaimu nafasi hiyo.

Mmoja wa askari hao, akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema kwa ujumla wao wanashangazwa na jinsi Nyalandu alivyomwondoa kazini Prof Songorwa licha ya kuwa alikuwa mtendaji mzuri aliyejali wafanyakazi na kuweka uzalendo mbele.

"Profesa Songorwa alikuwa Pori la Selous kufanya doria siku tatu kabla ya kuondolewa kazini, alishirikiana na askari, hatua ambayo ni nadra sana kufanywa na viongozi," alisema mmoja wa askari hao

Alisema endapo Rais Jakaya Kikwete hatatengua uamuzi uliofanywa na Nyalandu, watafanya mgomo ambao utasababisha tembo kuuawa.

"Huyu mtu amekaa wizarani kwa mwaka mmoja tu, amejitahidi kudhibiti matumizi mabaya ya fedha, anajituma kiasi cha kulala porini, lakini leo anaondolewa katika kazi bila sababu za kueleweka
. Sisi tunahisi kuna jambo hapa," alisema askari huyo huku akichagizwa na wenzake.

Walisema wana wasiwasi kuwa kuondolewa kwa Profesa Songorwa kumesababishwa na utendaji wake mzuri hasa kudhibiti Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori (TWPF) ambao pengine umesababisha baadhi ya watendaji ndani ya wizara waliokosa masilahi kupeleka taarifa za uongo kumchongea Profesa Songorwa.

Askari hao walisema utendaji wa Profesa Songorwa ulikuwa wa pekee kwa aina yake na aliweza kuendesha kitengo cha kiintelijensia kilichogundua baadhi ya wafanyakazi wa maliasili kujihusisha na ujangili.

"Aliweza kuwagundua wafanyakazi wa wizara ambao ni majangili na majina anayo kwa nini asiachwe amalize kazi yake, badala yake anafukuzwa bila kosa." Alisema mmoja wao.

Hata hivyo, Nyalandu alikanusha tuhuma na lawama zilizorushwa kwake kuwa amewapangua wakurugenzi kinyume na taratibu, akisisitiza kuwa alichukua uamuzi huo kwa sababu ya kushindwa kutekeleza majukumu yao.

0 Responses to “PANGUA PANGUA MALIASILI YAIBUA MAPYA.”

Post a Comment

More to Read