Sunday, March 16, 2014

RAGE ATANGAZA KUNG"ATUKA SIMBA.




MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, jana ametangaza rasmi kwamba hatagombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Mei 4 mwaka huu.

Hata hivyo Rage kabla ya kutangaza maamuzi yake ya kutotetea cheo hicho katika uchaguzi mkuu ujao, wanachama wa klabu hiyo walianzisha vurugu katika mkutano mkuu huo uliotishwa maalumu kwa ajili ya kufanya marekebisho wa katiba kutokana na kiongozi wao huyo kuwaita ‘mbumbumbu’.

Kufuatia kauli hiyo, Rage, alilazimika kuwaomba radhi wanachama hao zaidi ya 571 waliohudhuria mkutano huyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
“Napenda kuwaomba radhi wanachama wenzangu kutokana na nilivyosema tuache umbumbumbu, lakini sikuwa namaanisha kama wengi wenu mlivyoelewa,” alisema Rage.

Licha ya kusema hatagombea tena uongozi, Rage, alisema ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Simba na atatoa mchango wake ili kufanikisha maendeleo.
“Nitatoa mchango wangu wa hali na mali, sina ugomvi na mtu yoyote na bado nina mapenzi na Simba,” aliongeza.

JK ACHANGIA UWANJA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, jana alitangaza kuipa Simba Sh. milioni 30 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Uwanja wake unaotarajiwa kujengwa katika eneo la Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Rage amesema kwamba Rais Kikwete alimueleza ahadi hiyo leo Jumapili asubuhi muda mfupi kabla ya kuelekea katika mkutano wa marekebisho ya katiba.
Rage alisema kuwa Rais huyo pia aliwatakia wanachama wa Simba heri na majadiliano ya amani.

Amesema kuwa alitumia nafasi hiyo kumuomba awasaidie kupata hati ya eneo la Uwanja wao lililoko Bunju ambalo tayari uongozi umeshalipia gharama ya Sh. milioni 50.

“Na alikubali kutusaidia na katika kuonyesha yeye (Kikwete) kuwa ni mwanamichezo, ameahidi kutupatia Sh. milioni 30 ili kufanikisha ujenzi wa uwanja,” Rage alisema.

Aliongeza kuwa uongozi wa Simba unatarajia kuanza kuufyeka uwanja huo kwa gari maalumu la kulimia ili waweze kutimiza ahadi ya kuanza kuutumia uwanja huo kwa mazoezi kabla ya siku 100 walizotangaza  hazijamalizika.

“Kwa niaba ya Klabu ya Simba tunamshukuru Rais kwa msaada huo, kweli ameendelea kudhihirisha yeye ni mpenzi wa michezo nchini,” Rage amesema.

Vile vile amesema Kamati ya Utendaji ya Simba juzi iliingia mkataba na Benki ya Posta Tanzania (TPB) kwa ajili ya kutoa kadi maalumu kwa mashabiki wa klabu hiyo na awamu ya kwanza wanatarajia kuingia Sh. milioni 300.

Amesema shabiki anayetaka kujiunga na mfumo huo ambao pia atakuwa amefungua akaunti kwenye benki hiyo atalazimika kulipia Sh. 5,000 na Sh. 3,000 zitaingizwa kwenye mfuko wa klabu, Sh. 1,000 itakuwa ni gharama za benki na kiasi kilichobakia ndiyo itakuwa kianzio chake kilichobaki.
…………………………………..
FEDHA ZA OKWI
Mwenyekiti huyo aliyeingia madarakani aliwaambia wanachama wa Simba kwamba bado uongozi wake haujapokea malipo ya Dola za Marekani 300,000 kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi.

Amesema fedha hizo zikiingia pamoja na nyingine zaidi ya Sh. milioni 216 (hakusema ni za nini) watazikabidhi kwa uongozi mpya utakaoingia madarakani.
Aliwataka wanachama wa Simba kuwa watulivu na wasisikilize maneno yanayozungumzwa pembeni kuhusiana na fedha hizo.

0 Responses to “RAGE ATANGAZA KUNG"ATUKA SIMBA.”

Post a Comment

More to Read