Monday, March 17, 2014

SAKATA LA FOLENI,SERIKALI SASA YANYOOSHA MIKONO.




Serikali imenyoosha mikono ikisema ni shughuli ngumu kumaliza kabisa tatizo la foleni za magari nchini na hasa Dar es Salaam, bali kinachowezekana ni kuzipunguza tu.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Greyson Lwenge amesema “Hakuna dawa ya msongamano, asikudanganye mtu, tunaweza kupunguza tu lakini si kumaliza. Hebu fikiria, idadi ya watu inaongezeka, magari yanaongezeka kila siku.”
Amesema tatizo kubwa linalochangia msongamano huo ni muundo wa jiji ambao umeruhusu maeneo ya biashara kuwekwa sehemu moja.

“Watu wote asubuhi wanaelekea Posta na Kariakoo na jioni wanatumia barabara tatu tu kurudi katika makazi yao,” alisema.
Lwenge alitoa suluhisho la kupunguza msongamano huo na kusema kuwa, ni vyema jiji likavunjwa na miji mingine mipya iundwe.

“Muundo wa jiji ndicho chanzo cha haya, kwa hiyo ni lazima tubadili mfumo wa jiji kwa kulibomoa na kulibadili kabisa. Kwa kifupi tulihamishe,” amesema.

Alisema suluhisho ni kuhamisha maeneo makubwa ya biashara kwa kuyapeleka nje ya jiji, zikiwamo huduma zinazopatikana katikati ya jiji nazo zisogezwe ili watu wasiwe wanaelekea eneo moja kwa wakati mmoja.

Suluhisho jingine alilotoa Lwenge ni kuhusu mfumo wa usimamizi wa magari (Traffic Light) ambapo alisema badala ya kutumia askari wa usalama barabarani ni vyema ikatumika teknolojia ya ‘Traffic jam Cameras.’

“Tuwe na mfumo wa kiteknolojia ambao utasimamia magari yote katika barabara zote za jiji kwa kutumia kamera moja na mfumo mmoja,” amesema.
Amesema Serikali ipo mbioni kuanza kutumia mfumo huo wa kusimamia magari barabarani kama njia ya kupunguza msongamano.

Hata hivyo, Lwenge alisisitiza kuwa, njia zote hizi ni za kupunguza tu msongamano na wala si kuumaliza. “Hata Jiji la London wanatumia mbinu zote hizi lakini bado kuna msongamano,”amesema.
Mbunge wa kuteuliwa na Rais, James Mbatia naye alisema hakuna suluhisho la kudumu la kumaliza msongamano na kutaka kufanyiwa kazi utashi wa kisiasa pamoja na kujenga mji mpya.

0 Responses to “SAKATA LA FOLENI,SERIKALI SASA YANYOOSHA MIKONO.”

Post a Comment

More to Read