Monday, March 17, 2014

AKATA RUFAA KWA KUTORIDHISHWA NA UAMUZI WA KUMFUNGIA MWAKA MMOJA CCM




 Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amekata rufaa Kamati Kuu ya CCM kupinga adhabu ya onyo kali aliyopewa na chama kutokana na madai ya kuanza kampeni za urais mapema kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Akizungumza mjini Dodoma jana, Sumaye amesema kwa ufupi hakuridhishwa na adhabu hiyo na kuthibitisha hilo, tayari amekata rufaa.

Hata hivyo, amesema hadi jana hakuwa amepata mrejesho wowote kwa sababu kanuni hazielezi ni muda gani anatakiwa kuwa amepewa taarifa kuhusu rufaa hiyo.

Sumaye na wanachama wenzake, Edward Lowassa, Bernard Membe, Stephen Wassira, William Ngeleja na January Makamba walitiwa hatiani kwa kuanza kampeni mapema, hivyo kupewa onyo linalokwenda sambamba na kutowania nafasi yoyote ndani ya chama kwa miezi 12.

“Siwezi kuwazungumzia wenzangu, nazungumza kwa upande wangu, sikuridhishwa na adhabu hii na nimeshakata rufaa ingawa sijapata majibu yoyote, naendelea kusubiri,” alieleza Sumaye.

Waziri Sumaye alikataa kuzungumzia hali ya utekelezaji wa adhabu hiyo, akisema anachosubiri ni mwitiko wa rufaa yake aliyoiwasilisha Kamati Kuu ya CCM, mwanzoni mwa mwezi huu. “Sina kumbukumbu nzuri ilikuwa tarehe ngapi, lakini ni mwezi huu wa tatu.”

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa juu ya rufaa hiyo amesema hana taarifa zaidi ya habari hizo kuzisikia kutoka kwa mwandishi.

0 Responses to “AKATA RUFAA KWA KUTORIDHISHWA NA UAMUZI WA KUMFUNGIA MWAKA MMOJA CCM”

Post a Comment

More to Read