Monday, March 17, 2014

DAKIKA 60 KWA WARIOBA SIYO HAKI.




Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Julius Mtatiro amepinga hatua ya uongozi wa Bunge hilo kumpa saa moja Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba kwa wajumbe leo. Ufuatao ni waraka huo wa Mtatiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha CUF.
Kanuni ya 47(a) ya Bunge Maalumu la Katiba inaeleza kuwa “Mwenyekiti (wa Bunge Maalumu la Katiba) baada ya kushauriana na Mwenyekiti wa Tume (ya Mabadiliko ya Katiba), watapanga muda unaofaa kwa ajili ya Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalumu.”

Jambo la ajabu ni kuwa, jana (juzi) Jumamosi, Samueli Sitta ametangaza kuwa kesho (leo) Jumatatu jioni, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba atawasilisha Rasimu kwa muda usiozidi dakika 60.

Taarifa za uhakika tulizonazo ni kuwa Mwenyekiti wetu wa Bunge Maalumu hajawasiliana na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kupanga muda kama kanuni inavyoelekeza.

Hata hivyo, alipoulizwa jana kuhusu kukutana na kujadiliana muda, Jaji Warioba alisema aliwasiliana na Mwenyekiti wa Bunge kuhusu muda na kwamba unatosha hivyo kuwataka wajumbe wasiwe na shaka juu ya hilo.

Ikumbukwe kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imefanya kazi kubwa sana kwa miezi zaidi ya 20. Kazi hiyo inahitimishwa kesho (leo) Jumatatu Machi 17, mwaka huu saa 10.00 jioni wakati Jaji Warioba atakapoiwasilisha rasimu na kuielezea ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.

Ikiwa Jaji Warioba anapewa dakika 60 tu kuelezea kwa kina rasimu Sura 17, Ibara 271 na Kurasa 148. Jambo hili haliwezekani na halikubaliki hata kidogo. Kwa maoni yangu, Kazi iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa miezi 20, haiwezi kuwasilishwa bungeni kwa dakika 60.

Bunge Maalumu la Katiba limetumia wiki tatu kutengeneza kanuni, linatumia siku tatu kwa wajumbe kuapa, eti Bunge hilohilo halina saa tano au dakika 300 kwa ajili ya kumsikiliza Jaji Warioba! Binafsi napata wasiwasi mkubwa ikiwa tutakwenda mbele namna hii.

Nchi ya Ghana ilipokuwa katika hatua hii, Bunge lao la Katiba lilitenga siku mbili kwa ajili ya kuisikiliza Tume ya Katiba ikiwasilisha rasimu ya Katiba, sisi hatuna hata siku moja kwa ajili hiyo? Nchi hii tuna matatizo gani?

Samuel Sitta ameaminiwa na wajumbe wengi wa Bunge Maalumu, nikiwamo, nadhani Watanzania wengi wana imani naye katika kusimamia suala hili. Asianze kujisahahu na kufanya vitendo ambavyo vitafanya tutilie shaka nia yake.

Kiongozi mzuri ni yule anayetenda kulingana na makubaliano na anayetenda kwa nia safi ambayo inaaminiwa.

Hoja kubwa aliyoitumia katika kufanya uamuzi huo ni kwamba, kwa taratibu za mabunge, hoja yoyote huwasilishwa tu bila ya ufafanuzi.

0 Responses to “DAKIKA 60 KWA WARIOBA SIYO HAKI. ”

Post a Comment

More to Read